Rais Jonathan anaongoza katika matokeo ya uchaguzi
18 Aprili 2011Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa jana Jumapili. Tume huru ya uchaguzi ya Nigeria bado inasubiri matokeo kutoka kwenye jimbo moja na maeneo mengine kadhaa.
Idadi kubwa ya karibu watu milioni 73 na nusu waliojiandikisha kupiga kura walijitokeza katika uchaguzi huo wa rais uliofanyika Jumamosi iliyopita.
Mpinzani mkuu wa Rais Jonathan, Muhammadu Buhari ambaye ni kiongozi wa zamani wa kijeshi, amepata kiasi kura milioni 11, nyingi zikiwa zimepigwa katika maeneo ya kaskazini ya nchi hiyo.
Katika taarifa ya awali ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi huo kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi-ECOWAS umeuelezea uchaguzi huo katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika kuwa huru, wa haki na kuaminika. Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa leo.