1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Jose dos Santos wa Angola aamua kung'atuka

Oumilkheir Hamidou
3 Februari 2017

Rais wa Angola Jose Edouardo dos Santos amethibitisha hatogombea tena wadhifa huo uchaguzi mkuu utakapoitishwa mwezi Agosti mwaka huu. Dos Santos anang'atuka baada ya kuitawala Angola kwa muda wa miaka 37

Angola Jose Eduardo dos Santos
Picha: Getty Images/AFP/A. Pizzoli

Miongoni mwa viongozi waliotawala kwa muda mrefu kabisa barani Afrika, basi Jose Edouardo Dos Santos ni wa pili: Ametanguliwa na Teodoro Obiang Nguema tu wa Guine ya Ikweta. Jose Edouard dos Santos anaiongoza Angola tangu septemba 20 mwaka 1979. Kabla ya hapo Angola ilitawaliwa na rais mmoja tu, Agostinho Neto aliyeiongoza nchi hiyo hadi uhuru kutoka Ureno mwaka 1975. Matatizo ya afya ya Dos Santos yamezidi mnamo miaka ya hivi karibuni kwa namna ambayo uvumi ulizagaa atang'atuka.

Kama wadadisi walivyoashiria decemba mwaka jana, dhana hizo sasa zimethibitishwa : waziri wa ulinzi Joâo Lourenco ndie aliyeteuliwa  na kamati kuu ya chama tawala cha MPLA kukiongoza chama hicho uchaguzi  mkuu utakapoitishwa Agosti mwaka huu. Uamuzi huo umetangazwa na mwenyewe Dos Santos , mashuhuri kwa jina la "Zedu"mkutano wa chama ulipofunguliwa hii leo.

"Waangola wengi watashuhudia tukio la kubadilishwa rais" amesema Alex Vines wa kituo cha kutafakari cha Chatham nchini Uingereza.

 

Jenerali mstaafu Joâo Lourenco atakaekamata nafasi ya Edouaardo dos SantosPicha: Getty Images/AFP

Ni mabadiliko muhimu katika historia ya Angola

 

,Mwanaharakati wa upande wa upinzani nchini Angola, Nuno Dala anazuangalia uamuzi wa kumteuwa  Lourenco kwa jicho la wasi wasi na kusema: "Kutokana na uamuzi huo madaraka yataendelea kudhibitiwa na wanajeshi kwakua Lourenco binafsi ni jenerali."

Jenerali huyo mstaafu ataiongoza Angola ikiwa chama tawala cha MPLA ndicho kitakachoibuka  na ushindi.Na kila kitu kinaashiria hali hiyo.

Katiba ya Angola haizungumzii kuhusu uchaguzi wa rais, lakini inafafanua wadhifa wa rais unashikiliwa na mwenyekiti wa chama kinachoshinda katika uchaguzi mkuu.

Utaratibu wa kipindi cha mpito umeshathibitishwa na Dos Santos. Hali hiyo itamaliza uvumi wa wale wanaohisi rais Dos santos anaweza kubadilisha maoni yake, anasema Alex Vines.

 

Mwanasiasa wa upinzani Abel ChivukuvukuPicha: DW/J. Carlos

Wapinzani hawatarajii mabadiliko yoyote

 

Atakapong'atuka mpiganaji huo wa zamani wa msituni, aliyekuwa akifuata siasa za mrengo wa kushoto za Marx, utafunguliwa pia ukurasa mpya katika historia ya Angola, ingawa wapinzani hawatarajii mabadiliko makubwa.

Dos Santos aliyemchagua binti yake Isabel, anaetajikana kuwa mwanamke tajiri kupita wote barani Afrika, kuwa mkurugenzi wa kampuni la mafuta la Sonagol, anang'atuka akiiacha Angola katika hali ya umaskini kupita kiasi na kuzongwa na mzozo wa kiuchumi uliosababishwa na kuporomoka bei ya mafuta ulimwenguni. Angola ni msafirishaji mkubwa wa mafuta kutoka bara la Afrika.

 

Mwandishi:Johannes Beck/Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW