Rais Kagame ajitokeza na kukomesha uvumi kuhusu kifo chake
7 Septemba 2020Akizungumza na shirika la utangazaji la taifa nchini Rwanda Rais Kagame amesema kwamba afya yake haina matatizo lakini akaonya wapinzani wa serikali yake walioko ambayo amewataja kama ndiyo wamekuwa wakisambaza uvumi huo.
Rais Paul Kagame ameyasema hayo alipokuwa akizungumza kutoka Ikulu yake mjini Kigali katika mazungumzo yaliyorushwa mubashara kupitia Radio na Televishei ya taifa. Kauli yake imekuja wiki chache baada ya kuenea wimbi la taarifa mitandaoni kwamba alikuwa amefariki dunia.
Kupitia mtandao wa Youtube mpinzani mmoja wa serikali ya Rwanda Kasisi Nahimana Thomas ambaye anaishi uhamishoni nchini Ufaransa alisema kwamba Rais Kagame hayuko tena. Ni taarifa ambayo ilipewa uzito nchi za nje huku ndani ya Rwanda ikipuuziliwa mbali.
"Hayo nimeyasikia si siku nyingi zilizopita, si kuhusu afya tu kuwa hafifu, hao na walikwenda mbali na kutangaza kifo changu, lakini kwa kuwa wote mnaishi huku kuna msemo usemao kwamba ukimtakia baya mama wa kambo, linamtokea mama yako," amesema Nahimana.
Kwa mara ya kwanza wiki moja baada ya kukamatwa Paul Rusesabagina, ambaye mchango wake wa kuwaokoa watu wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ulichezwa katika filamu ya Hotel, huku lakini mchango wake huo ukitiliwa mashaka nchini Rwanda, Rais Paul Kagame amezungumzia kukamatwa huko akisema.
"Mnatambua kundi la FLN na MRCD mnatambau vitendo vyao,huyu anatambulika kama kiongozi wao na mara kadhaa amejigamba mashambulizi yao, na mtambau pia watu wanaouawa maeneo ya Nyaruguru, Nyamagabe na mahali pengine, hapa kuna hoja shutuma anayotakiwa kujibu. Amesema Rais Kagame.
Paul Rusesabagina ana uraia wa Ubelgiji lakini alikuwa na hati za kuishi Marekani hadi alipokamatwa wiki iliyopita ijapokuwa hadi sasa haijulikana ni kwa namna gani alikamatwa na kurejeshwa Rwanda.
Rais Paul Kagame pia amezungumzia uhusiano wa Rwanda na Jamhuri ya Kimokrasia ya Kongo hasa kuhusu ripoti ya watalaam wa umoja wa mataifa ambayo imezua utata na majibizano kati ya Rwanda na baadhi ya mashirika binafsi kule Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Amesema wanaochochea mzozo huo ni wale wanaotaka kuziweka shutuma zote juu ya Rwanda, huku wakificha dhima yao katika matatizo yaliyotokea DRC.
Amegusia vile vile uhusiano wa Rwanda na mataifa ya Uganda na Burundi ambayo kwa miaka ya hivi karibuni yamekuwa mahasimu wakubwa wa Rwanda, akasema kwamba mpaka sasa bado una doa ijapokuwa kwa upande wa Burundi alijaribu kuufufua ila upande mwingine ukaonekana kupuuza.