Rais Karzai wa Afghanistan akubali kufanyike duru ya pili ya uchaguzi
21 Oktoba 2009Miezi miwili ikiwa imepita tangu Wa-Afghanistan waende katika vituo vya upigaji kura, sasa ni wazi kwamba itawabidi wafanye hivyo tena. Katika mkutano wa waandishi wa habari, rais aliye madarakani, Hamid Karzai, alitangaza kwamba kutakuweko duru ya pili ya uchaguzi. Hiyo ina maana kwamba Hamid Karzai amekiri kwamba hajapata wingi ulio wazi katika duru ya kwanza. Kwa hivyo, hajabakia na chaguo lengine isipokuwa kukubali ifanyike duru ya pili:
" Nalitolea mwito taifa leo kuichukuwa hii kama ni nafasi kwa mashikamano yetu yaongezeke na kuipeleka nchi yetu mbele. Nawaomba watu washiriki katika uchaguzi huo."
Hamid Karzai yaonesha amekosea chupu chupu kupata wingi ulio wazi katika uchaguzi uliopita; lakini, hata hivyo, ndio ameshindwa kukifikia kiunzi cha zaidi ya asilimia 50 ya kura. Msemaji wa tume huru ya uchaguzi alitangaza kwamba rais huyo alipata asilimia 49.67 ya kura. Juzi, jumatatu, taasisi nyingine, tume huru ya kuchunguza malalamiko ya uchaguzi, iliamuru kwamba idadi kubwa ya kura lazima zibatilishwe kutokana na malalamiko ya udanganyifu. Suali kubwa lilikuwa: jee Karzai atapata chini ya asilimia 50 ya kura, na ikiwa ndio, jee yeye mwenyewe ataikubali hali hiyo?
Jamii ya kimataifa iliongeza mbinyo katika siku za karibuni kwa kipenzi huyo wa zamani wa nchi za Magharibi. Kwa hivyo, Karzai pia akasifiwa na Seneta wa Kimarekani, John Kerry, ambaye alikuwa ubavuni mwake katika mkutano huo muhimu na waandishi wa habari huko Kabul.
"Rais Karzai alikuwa na wasiwasi mkubwa juu ya mwenendo wa uchaguzi huo. Lakini leo amejitokeza kama mwanasiasa, hivyo ameamua kushindana tena na nchi kuimarisha. Hivyo ameikubali katiba na sheria."
Katiba inasema kwamba kuweko marudio ya uchaguzi pindi hakuna mtetezi aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura katika duru ya kwanza. Wachunguzi wa mambo walikuwa na wasiwasi mkubwa kama kweli duru ya pili ya uchaguzi itafanyika. Katika sehemu kubwa za Afghanistan majira ya baridi yenye barafu yanaanza kidogokidogo kusogea. Kama watu wengi watakwenda kupiga kura mara hii kama ilivyokuwa katika duru ya kwanza ni suali ambalo kwa sasa haliwezi kupatiwa jibu. Na pia kama katika duru ya pili mambo yote ya zoezi la upigaji kura yatakwenda sawa. Seneta John Kerry alisema:
"Haiwezi kila wakati kusisitizwa kwamba itabidi kukabiliana na mitihani ya kuufanya uchaguzi huo katika hali ngumu ya usalama."
Seneta Kerry alishikilia pia kwamba sasa ule wakati wa kutojuwa sana nini kitatokea umegeuka kuwa wakati wa kuweko nafasi kubwa. Kwa hakika, kulikuweko malalamiko kutoka duniani kwamba rais Karzai alikuwa anang'ang'ania kiti ambacho anakikalia kutokana na udanganyifu mkubwa uliofanyika katika uchaguzi. Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa, Kai Eide, pia alitoa pongezi kwamba taasisi zilizoshiriki katika uchaguzi huo zimefanya kazi.
" Katika nchi ilio na demokrasia changa, ni muhimu kwamba vyombo vinavoisaidia demokrasia hiyo vifanye kazi."
Kwa vyovyote, Wa-Afghanistan wameweka wazi kwa vile sasa wamelitanzua lile suali lililokuweko: jee kutafanywa uchaguzi au hakutafanywa. Nani atakuwa rais wao mpya, ni jambo ambalo kwa sasa hawalijui.
Mwandishi: Küstner, Kai /Othman Miraji/ZP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman