1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Kenyatta amtaka makamu wake William Ruto kujiuzulu

Shisia Wasilwa24 Agosti 2021

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemtaka Makamu wake William Ruto aliyehudumu naye kwa miaka tisa kujiuzulu badala ya kuishambulia serikali ambayo anaitumikia.

Kenia President Kenyatta Rede Terroranschläge 02.12.2014
Picha: AFP/Getty Images/S. Maina

Rais Kenyatta aliyeonekana kuhamaki aliyasema hayo kwa mara ya kwanza tangu, Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali, Mpango wa Maridhiano wa Taifa - BBI, uliolenga kubadilisha Katiba kwa kuitaja kuwa iliyokiuka sheria. Matamshi yake kwa mara nyingine yakiongeza kaa la moto, kati yake na makamu wake William Ruto, ulioanzishwa na ushirikiano wake na kiongozi wa ODM Raila Odinga. Kiongozi wa Taifa la Kenya, amemkosoa makamu wake ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa serikali, ambaye alisema anawachanganya wapiga kura kwa matendo yake. Ruto amekisajali chama chake cha United Democratic Alliance, licha ya kuwa katika chama tawala cha Jubilee na kubainisha kuwa atagombea kiti cha urais. 

"Kitu cha heshima cha kufanya ni kujiuzulu na kuruhusu wanaotaka kuendelea kuendelea, kisha ufikishe ajenda yako kwa wananchi, jambo ambalo hufanyika katika mazingira ya demokrasia. Kwa upande mmoja huwezi ukasema huondoki na wakati huo huo unasema sikubaliani.”

Rais Kenyatta na Raila Odinga na William RutoPicha: AFP/T. Karumba

Kitumbua cha Ruto kiliingia mchanga wakati alipoanza kuzunguka nchi nzima kupiga siasa, huku rais akimwonya mara kwa mara kuwa ulikuwa wakati wa kuwahudumia wapiga kura, jambo ambalo Ruto aliliipuuza. Huku akimuunga Ruto kwa kuunda msingi wa siasa za mwaka ujao kuwa haki yake ya kikatiba, Rais Kenyatta alimkosoa kuhusu njia anayotumia kufikia malengo hayo. Washirika wa karibu wa siasa wa Ruto walitimuliwa kwenye ngazi za juu serikalini, baada ya Ruto kuendelea kupiga siasa. Kenyatta amebainisha kuwa hatayumbishwa na misukosuko inayoshuhudiwa katika kutimiza malengo yake.

Rais Kenyatta ambaye anakamilisha utawala wa mihula ya miwili ya miaka kumi, amepuuzilia mbali mjadala wa kuahirisha tarehe ya uchaguzi mwakani, huku washirika wake wa karibu wakimsihi kubakia madarakani. Katiba ya Kenya inaeleza kuwa uchaguzi mkuu na ule wa wabunge utafanyika kila Jumanne ya kwanza ya mwezi Agosti kila baada ya miaka mitano. Uchaguzi mkuu ujao utafanyika tarehe tisa, Agosti, mwaka 2022. Mahakama ilipotengua Mpango wa Maridhiano wa Taifa, rais amesema kuwa ni Wakenya waliopoteza, huku Ruto akisherehekea ushindi huo.

"Uamuzi wa Mahakama, unadhihirisha kuwa taifa la Kenya, linaongozwa kwa misingi ya sheria, sio misingi ya binadamu.”

Aidha matamshi ya rais yanajiri huku Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia Joe Mucheru akimshambulia Ruto kwa kutoa ahadi kwa vijana na kutumia injili kuwashawishi wananchi. Mucheru amesema kuwa Ruto anatumia mbinu zilozipitwa na wakati. Ruto ameahidi kuunda serikali kwa kuwajumuisha watu wanyonge katika jamii ili kujenga uchumi na taifa dhabiti. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW