Rais Kenyatta azindua ripoti rasmi ya maridhiano 'BBI'
26 Oktoba 2020Rais Uhuru Kenyatta amewalaumu viongozi kwa kuchangia kuongezeka kwa ukabila nchini humo. Ameongeza kusema kuwa, iwapo suala la ukabila halitaangaziwa kwa uangalifu, huenda likawa bomu litakalolipuka.
Safari ya kufanyika kwa kura ya maoni nchini Kenya, ilianza rasmi leo wakati zaidi ya Wakenya 6000 walipojumuika katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi, kwenye uzinduzi wa ripoti ya maridhiano ya BBI.
Ripoti hiyo ambayo imekuwa ikitayarishwa kwa kipindi cha miaka miwili sasa, na ambayo imeshabikiwa na viongozi wote waliopata nafasi ya kuhutubia, inapendekeza marekebisho kwenye muundo wa utawala wa serikali.
Ripoti ya BBI yapendekeza kuwepo wadhifa wa Waziri Mkuu Kenya
Ripoti hiyo inapendekeza kuwepo kwa nafasi za Waziri Mkuu na manaibu wake wawili. Waasisi wake wanasema sababu kuu ni kuzima ghasia za kila baada ya uchaguzi mkuu. Rais Uhuru Kenyatta amemtaka naibu wake Ruto kupunguza kampeni za siasa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo baadhi ya wachanganuzi wa siasa wanashikilia kuwa mapendekezo ya ripoti ya BBI yanampa rais mamlaka zaidi, kwani atakuwa na uwezo wa kumchagua na kumfuta kazi Waziri Mkuu. Aidha wapinzani wa ripoti yenyewe wanasema kuwa kuongezwa kwa nafasi za uongozi, kunaongeza mzigo kwa mlipa kodi. Naibu Rais William Ruto alianza kuzomewa alipojaribu kuvipinga baadhi ya vipengee alipokuwa akilihutubia kongamano hilo.
Aidha ripoti hiyo imependekeza kuboreshwa kwa serikali za majimbo kwa kuongeza mgao kwa asilimia 35 kutoka kwa asilimia 15. Uakilishi wa wanawake umepigiwa debe kwenye ripoti hii.
Raila awataka viongozi kuukabili ugonjwa wa ukabila
Katika majimbo 47, watachaguliwa maseneta wawili mmoja wa kike na mwingine wa kiume, huku gavana wa kiume akihitajika kumchagua naibu wa kike. Raila Odinga amewataka Wakenya kukabiliana na ugonjwa wa ukabila, ambao amesema umekuwa ukilitafuna taifa hasa wakati wa uchaguzi.
Mapendekezo mengine kwenye ripoti hiyo ni kuwepo kwa Waziri Mkuu, ambaye atakuwa kiongozi wa bunge na baraza la mawaziri kwa niaba ya serikali. Manaibu wake watakuwa kwenye baraza la mawaziri.
Kinyume na katiba iliyopitishwa mwaka 2010, ripoti ya BBI inapendekeza afisi ya kiongozi wa upinzani ambaye atawajibisha serikali. Kiongozi wa upinzani atakuwa mgombea wa pili kwenye uchaguzi mkuu ama atachaguliwa kutoka kwa muuungano wa vyama wenye asilimia 25 ya wabunge wote. Wakenya wanasemaje kuhusu ripoti hii.
Mchakato wa Ripoti hiyo ulianza wakati Rais Kenyatta na Raila walipoamua kuzika tofauti zao za siasa kwenye uchaguzi uliokumbwa na mvutano mwaka 2017, katika kile kilichoitwa kupeana mkono, au handshake.