1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Macky Sall akutana na rais mteule Diomaye Faye

29 Machi 2024

Kiongozi wa upinzani na rais mteule wa Senegal Bassirou Diomaye Faye, amepokelewa siku ya Alhamisi katika ikulu ya rais na rais anayeondoka madarakani Macky Sall.

Rais mteule wa Senegal Bassirou Diomaye Faye
Rais mteule wa Senegal Bassirou Diomaye Faye akizungumza na waandishi wa habari mjini Dakar: 25.03.2024Picha: Luc Gnago/REUTERS

Ikulu ya Senegal imesema viongozi hao wamejadiliana kuhusu masuala muhimu ya serikali pamoja na mipango ya sherehe za kuapishwa. Ushindi wa Faye mwenye umri wa miaka 44 unatarajiwa kuthibitishwa katika siku chache zijazo na hivyo kuchukua rasmi madaraka kabla ya tarehe pili Aprili.  

Faye na Sall wamekutana  baada ya wiki kadhaa za mzozo kuhusu mchakato wa uchaguzi, jambo linaloashiria makabidhiano ya haraka na ya amani katika taifa hilo la Afrika Magharibi ambalo limekuwa likisifika kwa utulivu wa kidemokrasia katika eneo ambalo limekumbwa na mapinduzi ya kijeshi.

Matokeo ya awali yampa Faye ushindi wa kishindo

Tume huru ya uchaguzi nchini Senegal ilitangaza siku ya Alhamisi matokeo ya awali ya uchaguzi ambayo yanampa ushindi wa kishindo mpinzani Bassirou Diomaye Faye ambaye amejipatia asilimia 54.28 ya kura, huku mgombea Amadou Ba akiambulia asilimia 35.79.    

Ushindi wa mpinzani huyo ambaye alikuwa gerezani siku kumi kabla ya kufanyika uchaguzi, sasa ni lazima uidhinishwe na Baraza la Katiba.

Rais wa Senegal anayemaliza muda wake Macky SallPicha: John Thys/AFP

Iwapo ushindi wa Faye utathibitishwa, jambo linalotarajiwa hivi karibuni, itakuwa ni mara ya kwanza kwa mpinzani kushinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais, tangu Senegal ijipatie uhuru wake mwaka 1960.

Soma pia: Faye analenga kuibadilisha Senegal kiuchumi kwa kutumia gesi na mafuta

Sall alizua mzozo wa kisiasa mwezi Februari baada ya kutangaza kuahirisha uchaguzi wa rais akielezea wasiwasi wa usalama katika taifa hilo lenye watu karibu milioni 18. Hatua hiyo ilizusha maandamano makubwa ya umma yaliyosababisha vifo vya watu wanne, kabla ya Mahakama ya Katiba kuamuru uchaguzi huo ufanyike tarehe 24 Machi,2024.

Rais wa Marekani Joe Biden amempongeza Bw. Faye anayetarajia kuwa rais wa tano pamoja na watu wa Senegal kwa kuzingatia misingi ya demokrasia. 

Maoni: Bassirou Diomaye Faye achaguliwa rais mpya wa Senegal

This browser does not support the audio element.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW