Rais Macky Sall apendekeza mswada wa msamaha Senegal
27 Februari 2024
Rais Sall alitangaza muswada wa msamaha kwenye hafla ya ufunguzi wa mazungumzo ya kitaifa. Akipendekeza kuwa mazungumzo hayo yanaweza kuiunganisha nchi kufuatia mzozo wa kisiasa uliopo hivi sasa.
"Katika ari ya maridhiano ya kitaifa, nitawasilisha mbele ya Bunge Jumatano hii katika baraza la mawaziri muswada wa msamaha wa jumla kwa vitendo vinavyohusiana na maandamano ya kisiasa yaliyofanyika kati ya 2021 na 2024. Hii itawezesha kutuliza uwanja wa kisiasa.", alisema Sall.
Kulingana na baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu, zaidi ya watu 1,000 wamekamatwa tangu 2021 wakati wa mzozo wa kuwania madaraka kati ya kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko na serikali. Hivi sasa kiongozi huyo wa upinzani, Ousmane Sonko na mgombea mbadala wa chama chake, Bassirou Diomaye Faye, wote wako gerezani.
Maoni mseto
Siku za hivi karibuni, mamlaka imewaachilia mamia ya wafungwa. Katika juhudi tu za kutuliza vurugu, Chuo Kikuu cha Cheikh Anta Diop katika mji mkuu Dakar pia kilifungua tena siku ya Jumatatu baada ya kufungwa kwa miezi kadhaa. Wazo la msamaha limeibua maoni mseto miongoni mwa wafuasi wa serikali na upinzani.
Baadhi ya wakosoaji wanahisi kwamba hatua hiyo haitawajibisha ukatili uliofanywa na waandamanaji, huku kambi ya upinzani ikihofia kuwa itatumika kuwaondolea hatia maafisa wa serikali na usalama kwa vifo vya waandamanaji.
Mapinduzi ya kikataiba ?
Uamuzi wa Februari 3 wa kuahirisha uchaguzi wa rais uliitumbukiza Senegal katika machafuko ya kisiasa, na watu wanne waliuawa kwenye ghasia hizo. Macky Sall, aliye madarakani tangu mwaka wa 2012, alisema alifuta uchaguzi wa Februari 25 baada ya kufutwa kwa baadhi ya wagombea kwenye daftari ya wagombea wa uchaguzi wa rais na hofu ya nchi hiyo kurejea kwenye machafuko kama ilivyoshuhudiwa miaka miwili iliopita.
Upinzani uliita hatua ya rais Sall ya kuahirisha uchaguzi kuwa mapinduzi ya kikatiba. Katika hotuba yake ya ufunguzi wa majadiliano ya kitaifa, Sall alisema kuwa hana mpango wa kugombea tena uchaguzi na pia hana ajenda ya kibinafsi.
Hata hivyo, Macky Sall alitilia shaka uwezekano wa kuandaa uchaguzi kabla ya mwisho wa muhula wake, April 2. Alipendekeza kura hiyo ifanyike mwanzoni mwa msimu wa mvua mwezi Juni au Julai.
Ni wagombea wawili tu kati ya 19 waliokubali mwaliko wa rais Macky Sall wa kushiriki mazungumzo ya kitaifa. Mmoja ya wagombea, Cheikh Tidiane Dieye, aliutaja mkutano huo kama kichekesho.