1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Macron aambukizwa corona

17 Desemba 2020

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameambukizwa virusi vya corona. Ikulu yake imesema hayo leo hali ambayo imewalazimisha maafisa wawili wakuu wa Ufaransa kujiweka karantini.

Frankreich Präsident Emmanuel Macron
Picha: Lewis Joly/AP Photo/picture alliance

Kwenye taarifa, ofisi ya Emmanuel Macron imesema kuwa rais huyo alipimwa punde tu dalili za ugonjwa huo zilipojitokeza kwake, na sasa atajiweka karantini kulingana na maagizo ya kitaifa. Ofisi yake imeongeza kuwa Macron atatekeleza majukumu yake akiwa nyumbani.

Yeye ndiye kiongozi wa nchi wa hivi karibuni kuambukizwa virusi vya corona, baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na Rais wa Marekani Donald Trump

Kuambukizwa kwake kumetokea wakati kuna changamoto, akijaribu kulikabili janga hilo katika nchi yake na pia akifuatilia kwa karibu mazungumzo ya biashara ya baada ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, pamoja na masuala mengine ya kimataifa.

Wiki iliyopita, Rais Macron alihudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Aidha siku ya Jumatatu, alikuwepo kwenye mkutano ulioandaliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, OECD mjini Paris. Tayari rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel ambaye pia alihudhuria kwenye mkutano huo wa Paris, amejiweka karantini.

Soma Zaidi: Mji wa Paris kutangaza tahadhari ya juu dhidi ya COVID-19


Viongozi waliokutana na Macron wajiweka karantini

Waziri mkuu wa uhispania, Pedro Sanchez naye atajiweka karantiniPicha: Reuters/File/S. Perez

Aidha, ofisi ya Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez imesema kuwa kiongozi huyo ambaye pia alikuwepo kwenye mkutano huo amejiweka karantini. Waziri Mkuu wa Ureno, Antonio Costa vilevile alikutana na Macron na hivyo naye ofisi yake imetangaza atajiweka karantini.

Hata hivyo, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula, von der Leyen hatajiweka karantini. Msemaji wake amesema von der Leyen hana mpango huo. Alikutana na Macron mapema wiki hii, lakini maafisa nchini Ufaransa wamesema hawakusogeleana karibu.

Ofisi ya Macron imesema ziara ya Macron kuelekea Lebanonwiki ijayo ambako amekuwa akishinikiza mabadiliko makubwa ya kisiasa kufanywa baada ya mlipuko mkubwa katika bandari ya Beirut mwezi Agosti, imefutwa kwa sasa baada ya kukutwa na virusi hivyo. Waziri Mkuu wa Ufaransa Jean Castex naye atajiweka karantini kwani alikutana na Macron hivi karibuni.

Ofisi ya Castex imesema hayo na kuongeza kuwa japo waziri huyo mkuu hajaonyesha dalili zozote za maambukizi ya virusi vya corona, hatahudhuria kikao cha seneti leo kuainisha mikakati ya serikali kuhusu chanjo katika vita dhidi ya janga la COVID-19.

Mke wa Macron Bi Brigitte vilevile atajiweka karantini, ingawa hajaonyesha ishara zozote. Ofisi ya spika wa bunge nchini Ufaransa, imesema Spika Richard Ferrand naye atajiweka karantini kwani alikutana na Rais Macron.

Viongozi wa dunia wamtakia Macron afueni ya haraka

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson ni miongoni mwa viongozi waliomtakia afueni ya haraka Macron.Picha: Alberto Pezzali/empics/picture alliance

Viongozi mbalimbali ulimwenguni wamemtumia Macron salamu za kumtakia shufaa ya haraka. Kwenye ukurasa wa Twitter, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameandika, nasikitika kusikia rafiki yangu Emmanuel Macron ameambukizwa virusi vya corona. Tunamtakia ahueni ya haraka.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Layen amesema yuko pamoja na Macron moyoni mwake. Kwenye ukurasa wa Twitter, von der Leyen amesisitiza kuwa wataendelea kushirikiana kutoa chanjo na kuwalinda raia wao na watalishinda janga la corona.

Putin asema yuko tayari kupokea chanjo ya Sputnik V

Katika tukio tofauti, Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema leo kuwa atapokea chanjo ambayo imetengenezwa na nchi yake haraka iwezekanavyo. Putin mwenye umri wa miaka 68 ameeleza kuwa umri wake umepita umri wa wale wanaoshauriwa kupokea chanjo hiyo iliyoanza kutolewa mwezi wa Agosti nchini humo. Ameelezea imani yake kuhusu chanjo hiyo iitwayo Sputnik Vakisema hadi sasa imethibitishwa kuwa salama na imara.

Putin amesema ana matumaini kuhusu mpango wa kampuni ya chanjo ya Uingereza Astra Zeneca kuichanganya chanjo yake na ya Urusi kutengeneza chanjo imara zaidi.

(AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW