Rais Macron aingilia kati mgogoro wa Lebanon na Saudia
10 Novemba 2017Rais wa Ufaransa Emanuel Macron amekutana na mwanamfalme wa Saudi Arabia jana usiku mjini Riyadh katika kile kilichoonekana kuwa ziara ya ghafla nchini humo katika wakati ambapo mwanamfalme huyo amekuwa katika harakati za kuimarisha mamlaka yake. Hayo yametokana na kuonekana msururu wa hatua za kamatakamata dhidi ya wana wa kifalme na wafanyabiashara, hatua ambayo ufalme huo wa Saudi Arabia unasema ni harakati dhidi ya rushwa.
Rais wa Ufaransa amekutana na mwanamfalme Mohammed Bin Salman punde baada ya kuwasili mjini Riyadh akitokea Dubai ambako alizungumza na waandishi habari na kusema kwamba kombora lililofyetuliwa na waasi wa kishia wa Yemen mwishoni mwa wiki dhidi ya Saudi Arabia kilikuwa bila shaka kitendo kilichosababishwa na Iran.Rais huyo wa Ufaransa akasema pia wamekuwa na mawasiliano yasiyokuwa rasmi na Saad al Hariri waziri mkuu wa zamani wa Lebanon aliyejiuzulu hivi karibuni akiwa Saudi Arabia. Lakini pia Macron akaongeza kusema kwamba hakuna ombi lolote lililotolewa la kutaka Hariri ahamishiwe Ufaransa. Kadhalika amesema wasiwasi mkubwa walionao ni uthabiti wa nchi hiyo ya Lebanon na kuona kwamba suluhisho la kisiasa linaweza kupatikana haraka.
Maelezo ya rais wa Ufaransa yamekuja wakati ambapo maafisa wawili waandamizi wa serikali ya Lebanon jana walisema kwamba serikali ya Saudi Arabia inamshikilia mateka waziri mkuu huyo wa zamani Saad al Hariri huku afisa mwengine wa huko huko Lebanon akiliambia shirika la habari la Reuters kwamba Saudi Arabia ilimlazimisha Hariri kujiuzulu wakati akiwa mjini Riyadh mwishoni mwa wiki iliyopita na kumuweka katika kifungo cha nyumbani. Waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Fouad Saniora amesisitiza kwamba ipo haja kwa Saudi Arabia kumuachia huru Saad Al Hariri.
''Kurudi kwa waziri mkuu wa Lebanon, kiongozi wa kitaifa na kiongozi wa vuguvugu la kisiasa Saad Hariri ni jambo la muhimu katika kuirudisha hadhi ya Lebanon na heshima katika nchi hii na nje. Na hili lifanyike kwa kuzingatia kikamilifu heshima ya uhalali wa Lebanon ambao unasisitizwa katika katiba na makubaliano ya Taif sambamba na heshima ya nchi za kiarabu na serikali za kimataifa. Muungano huu na mamlaka ya kisiasa nchini Lebanon zimehakikisha kumuunga mkono waziri mkuu Hariri na uongozi wake na wanafuata maamuzi yake kwa hali yoyote ile.''
Kutokana na mvutano huu kushika kasi Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yve Le Drian amesema leo kwamba anaamini Al Hariri hakuwekwa katika kifungo cha nyumbani nchini Saudi Arabia na wala hajawekewa kipingamizi chochote cha kutembea. Juu ya Hilo balozi wa Ufaransa mjini Riyadh jana alikutana na Hariri kabla ya ziara ya rais Macron mjini Riyadh.Lakini haijafahamika iwapo rais huyo alikutana na Hariri huko Riyadh.Le Drian anatarajiwa Saudi Arabia tarehe 16 mwezi huu na amepangiwa pia kwenda Iran baadae mwezi huu.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Josephat Charo