1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Macron apewa tuzo ya Charlemagne

Caro Robi
10 Mei 2018

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amemtaka Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kuchukua hatua madhubuti na za haraka za kuleta mageuzi katika Umoja wa Ulaya katika kipindi hiki kigumu.

Verleihung Internationaler Karlspreis an Macron
Picha: Getty Images/AFP/P. Stollarz

 Mwaka mmoja tangu kuingia madarakani Rais Macron ameeleza kuishiwa na subira juu ya Ujerumani ambayo imedhihirisha kujikokota katika kuridhia mapendekezo ya kufanyika mageuzi hasa katika kanda inayotumia sarafu ya euro ikiwemo kumchagua waziri wa pamoja wa fedha wa kanda hiyo na kutenga bajeti itakayochochea ukuaji wa kiuchumi.

Katika hafla ya kupewa tuzo ya Charlemagne inayotambua juhudi zake za kuhakikisha mshikamano na utangamano wa Umoja wa Ulaya, mjini Aachen, Ujerumani, Macron amemhimiza Kansela Merkel kuchukua hatua sasa badala ya kusubiri.

Ujerumani yatakiwa kuchukua usukani wa kuiongoza Ulaya

Macron amesisitiza umuhimu wa umoja huo kuzungumza kwa sauti moja hasa wakati huu ambapo Marekani imeamua kujiondoa kutoka mikataba mbali mbali muhimu kama makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Macron aidha amesema pamoja na vitisho vya rais wa Marekani Donald Trump dhidi ya washirika wake kuhusiana na nyongeza za kodi, Ulaya inahitaji kusimama pamoja na kuonesha nguvu zake sasa kuliko wakati mwingine ule.

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/AFP/P. Stollarz

Macron amesema iwapo watakubali nchi nyingine zenye nguvu wakiwemo washirikia kujiweka katika nafasi ya kuwaamulia masuala ya kidiplomasia, usalama na wakati mwingine kuwaingiza katika hatari basi nchi za Ulaya hazitakuwa tena huru na hazitakuwa na hadhi mbele ya macho ya umma.

Kwa upande wake, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye pia amehutubia katika hafla hiyo ya kumpa tuzo Macron, rais wa pili wa Ufaransa kupewa tuzo hiyo, ametilia mkazo suala la kuwa Ulaya haiwezi tena kuitegemea Marekani kama mshirika na kuongeza kuwa ni wakati kwa Ulaya kujiamulia wenyewe kuhusu masuala yenye umuhimu na kujitwisha kikamilifu jukumu la mustakabali wa nchi zao katika siku za usoni.

Merkel pia amekiri kuwa mazungumzo kuhusu mageuzi ya kiuchumi katika kanda inayotumia sarafu ya euro ni magumu hasa kati ya Ujerumani na Ufaransa lakini ameongeza kusema kuwa uchumi wa Ulaya lazima ufanywe kuwa endelevu.

Macron ameishutumu Ujerumani kwa kusita kutumia fedha pamoja na kujivuta kuhusu mipango yoyote ya kutumia raslimali za nchi tajiri kuzisaidia zile zinazosuasua kiuchumi. Macron na Merkel wameahidi kufikia mchakato wa pamoja kuhusu mustakabali wa Umoja wa Ulaya ifikapo mkutano wa kilele wa umoja huo unaotarajiwa mwezi ujao.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga