Rais Macron azuru China
8 Januari 2018Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anafanya ziara rasmi nchini China. Macron ameanza ziara yake katika sehemu iliyokuwa mwanzo wa njia ya kale inayoitwa ya hariri, hiyo ikiwa ishara ya kuukubali mpango wa China kuifufua njia hiyo maarufu ya kibiashara.
Akiwa na mkewe Brigitte, Rais Emmanuel Macron alianza ziara hiyo ya siku tatu kwa kutembelea eneo maarufu la wapiganaji wa Terracotta katika mji wa Xian, eneo la makumbusho ya Pagoda, eneo la waumini wa Budha pamoja na msikiti wa mji huo.
Ziara hiyo ya kwanza ya Macron barani Asia inafungua ukurasa mpya wa kidiplomasia, ambao umekuwa ukijikita tu barani Ulaya na Afrika.
Wito kwa Ulaya kushiriki katika mradi wa njia ya China ya Hariri
Katika hotuba yake katika mji wa kaskazini wa China X'ian, Macron amelihimiza bara Ulaya kushiriki katika mpango wa kuifufua njia ya China ya Hariri. Pia amewataka viongozi wa China na Ulaya kushirikiana, katika kupiga vita mabadiliko ya tabianchi na kuunga mkono maendeleo ya Afrika.
" Mpango huu unajumuisha kusikiliza, kupendekeza na kuimarisha ujenzi wa imani, ili kwa pamoja kujenga uaminifu na kuthaminiana, na kutokana ana ahayo nitakuwa nikizuru China angalau mara moja kila mwaka katika kipindi changu cha urais."
Ziara ya Macron ni ishara ya kukubali mradi mpya wa rais wa China Xi Jinping wa kuifufua njia ya hariri kwa lengo la kuiunganisha Ulaya na Asia kupitia barabara, reli na bahari. Mradi huo unatarajiwa kugharimu dola trilioni moja. Zamani njia hiyo ilitumika kusafirisha vitambaa, viungo vya chakula, mali na bidhaa nyinginezo kati ya mabara mawili.
Macron anadhamiria kubuni ushirikiano wa kimkakati na China kuhusu masuala kadhaa kama vile vita dhidi ya ugaidi, tabia nchi na amfanye Xi kuwa mshirika katika kuutekeleza mkataba wa tabia nchi wa Paris hasa baada ya Marekani kujiondoa.
Mikataba ya kibiashara kati ya Ufaransa na China
Mikataba kadhaa ya kibiashara kati ya Ufaransa na China inatarajiwa kusainiwa wakati wa ziara ya Macron, na serikali hizo mbili zinatarajiwa kutangaza mfuko wa uwekezaji wa dola bilioni 1.2 kati ya Ufaransa na China.
Mradi huo umezusha msisimko na wasiwasi, huku baadhi ya nchi za Ulaya zikiuona kama mpango wa China kuendelea kujipanua kibiashara. Japo kuwa Ufaransa ilikuwa ikichelea kuukubali, Macron aliukubali mradi huo.
Hata hivyo Macron ameonya kuwa mradi huo unapaswa kutekelezwa kwa msingi wa ushirikiano ulio sawa. Hapo alikuwa akizungumzia biashara iliyopitiliza ya China. Ufaransa ina upungufu wa euro bilioni 30 kibiashara kati yake na China.
Macron anatarajiwa kutoa hotuba kuu baadaye mjini Xian kuhusu mustakabali wa mahusiano kati ya Ufaransa na China
Macron na mkewe Brigette wanatarajiwa kukutana na Rais Xi na mkewe Peng Liyuan leo usiku.
Mwandishi: John Juma/AFPE/APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman