1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron na Scholz wataka Ulaya itakayosimama mbele ya Trump

22 Januari 2025

Ujerumani na Ufaransa zasema utawala mpya wa Marekani utaleta changamoto lakini Ulaya inapaswa kuwa imara kusimamia maslahi yake.

Frankreich Paris 2025 | Macron empfängt Scholz zu Gesprächen im Élysée-Palast
Picha: Mohammed Badra/AFP

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron na Kansela Olaf Scholz wamekubaliana kwamba nchi zao zinapaswa kuchukua hatua, ili kuwa na Ulaya imara.

Viongozi hao wawili wametowa msimamo huo katika mkutano wao wa pamoja mjini Paris, siku chache baada Donald Trump kuingia madarakani kwa mara nyingine kuiongoza Marekani.

Rais Macron na Kansela Scholz wakizungumza katika mkutano wao kasri la ÉlyséePicha: Mohammed Badra/AFP

Viongozi hao wawili wamefanya mazungumzo hivi leo mchana na kisha kukutana na waandishi habari katika ikulu ya Elysee na kwenye mkutano huo Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, alisema uongozi mpya wa Marekani  utaleta changamoto kubwa na kwa kiasi kikubwa hilo limeshaonekana waziwazi.

Lakini amesisitiza juu ya umuhimu wa Ulaya kubakia imara katika ulimwengu unaobadilika.

Rais Emmanuel Macron kwa upande wake amesema nchi za Ulaya, zikiwemo Ufaransa na Ujerumani huu ni wakati wanapaswa kuyalinda mamlaka yao kutokana na kurejea madarakani kwa rais Donald Trump.

"Kwakuwa sasa utawala mpya nchini Marekani umeshaingia madarakani,ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine,kwa Ulaya na kwa mataifa yetu mawili kuchukua majukumu yetu kikamilifu katika kuimarisha umoja,nguvu zetu na mamlaka ya Ulaya. Ulaya ambayo itazingatia mahusiano na Marekani lakini ambayo pia itafahamu namna ya kuyazingatia maslahi yake na kuyatetea kwa misingi na  maadili yake''

Rais huyo wa Ufaransa ametia msisitizo kwamba Ulaya hivi sasa inahitaji kuwa imara zaidi kupambania maslahi yake.

Na juu ya hilo amezungumzia umuhimu wa kuunga mkono sekta za utengenezaji  magari,chuma na viwanda vya kemikali miongoni mwa biashara nyingine za barani Ulaya.

Rais Macron na Kansela ScholzPicha: Ludovic Marin/AFP

Msimamo wa Kansela Olaf Scholz ni kwamba Ulaya haitokuwa waoga na kujificha badala yake itasimama wima na kuwa tayari kuwa washirika imara.

 "Ulaya haitojiweka nyuma na kuwa waoga bali itakuwa washirika walio imara na wenye kujiamini. Kwa misingi hii tutafanya kazi vizuri pamoja na Marekani na rais mpya wa nchi hiyo. NATO ni mfadhili mkubwa wa usalama barani Ulaya na katika mahusiano na Marekani. Katika miaka ya hivi karibuni, sisi Ulaya tumeshirikiana kwa kiasi kikubwa pamoja kuimarisha nguzo hiyo ya Ulaya ya NATO.''

Emmanuel Macron, rais mstaafu Joe Biden, Keir Starmer na Olaf Scholz mjini BerlinPicha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Scholz amekumbusha  kwamba Ulaya na Marekani zinafungamanishwa na historia ya muda mrefu ya urafiki na ushirika ambao ameuita ni msingi imara kwa mahusiano ya baadae.

Lakini pia akasema rais Trump  tayari ameshatangaza hatua kadhaa kwenye sera yake,hatua ambazo Scholz amesema Ulaya itazitathmini kwa kina kwa pamoja.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW