1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGabon

Rais Macron wa Ufaransa aanza ziara Afrika

1 Machi 2023

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameanza ziara ya Afrika ya Kati katika harakati mpya za kidiplomasia kujaribu kutafuta uhusiano na bara hilo.

Paris Rede Macron zu Afrikapolitik
Picha: STEFANO RELLANDINI/AFP

Ziara hii inajiri huku hisia za kuipinga Ufaransa zikiongezeka katika baadhi ya makoloni yake ya zamani.

Katika ziara hii rais Macron, atatua kwanza Gabon kwa mkutano wa kilele wa mazingira, kabla ya kuelekea Angola kisha Jamuhuri ya Kongo inayojulikana kama Kongo-Brazzaville na hatimaye amalizie ziara hiyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

SOMA PIA; Rais wa Ufaransa ziarani nchini Cameroon

Ziara ya Macron inajiri wakati ambapo kuna wasiwasi nchini Ufaransa kuhusu kuongezeka kwa ushawishi wa Urusi katika nchi za Afrika zinazozungumza Kifaransa, sambamba na ushawishi wa China barani Afrika ambao umekuwa ukionekana kwa miaka kadhaa.

Nchini Gabon, rais Macronatahudhuria Mkutano wa Kilele kuhusu kuhifadhi misitu duniani kote pamoja na bonde kubwa la Mto Kongo.

Uhusiano na uwajibikaji kwa pande zote

Picha: Chris Jackson/AFP/Getty Images

Katika hotuba yake kuhusu sera ya Ufaransa kwa Afrika siku ya Jumatatu Macron alitoa wito wa uhusiano na uwajibikaji kwa pande zote, katika masuala mbalimbali yakiwemo yanayohusu hali ya hewa.

Lakini mwanaharakati wa mazingira wa Gabon Marc Ona Essangui aliiambia AFP kuwa ana wasiwasi ziara ya Macron itaondoa lengo kuu la mkutano wa kilele wa msitu wa mvua wa uhifadhi wa mazingira na badala yake watu wa Gabon wanaweza kuuona uwepo wake kama msukumo wa kisiasa kwa Rais Ali Bongo Ondimba katika maandalizi ya uchaguzi wa rais baadaye mwaka huu.

SOMA PIA; Viongozi wa Kiafrika wakutana na Macron

Macron amesisitiza kuwa Afrika ni kipaumbele katika muhula wake wa pili, na mwezi Julai alikwenda Cameroon, Benin na Guinea-Bissau.

"Mantiki ni kwamba mtindo wetu usiwe moja ya kambi za kijeshi kama zilivyo sasa. Uwepo wetu utakuwa sehemu ya mfumo wa vituo, shule na vyuo ambavyo vitasimamiwa kwa pamoja, na vitafanya kazi na wafanyikazi wa Ufaransa, ambao Watasalia katika ngazi za chini, na wafanyakazi wa Kiafrika. Kutakua na nafasi pia ya kuwakaribisha washirika wetu wengine kama Afrika itaridhia. Alisema rais  Macron.

Baada ya Gabon, rais Macronanaelekea koloni la zamani la Ureno, Angola, kama sehemu ya harakati za kuimarisha uhusiano wa Ufaransa na sehemu za Afrika zinazozungumza Kiingereza na Kireno.

Paris imetofautiana na mamlaka mpya za kijeshi katika makoloni ya zamani ya Mali na Burkina Faso na kuwaondoa wanajeshi wake kutoka nchi zote mbili kufuatia miaka ya kuwasaidia kupambana na makundi ya kijihadi.

Ufaransa na washirika wake wa Magharibi wanalishutumu kundi la mamluki la Urusi la Wagner, kwa kufanya kazi nchini Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati, na kuishutumu Urusi kwa kueneza habari potofu ili kudhoofisha maslahi ya Ufaransa katika bara hilo.

 

/AFP/Reuters

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW