1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ashawishiwa kutoyavunja makubaliano ya nyuklia ya Iran

24 Aprili 2018

Rais Donald Trump wa Marekani na mwenzake wa Ufaransa, Emannuel Macron, wanatarajiwa kuanza mazungumzo juu ya masuala mazito kama mkataba wa nyuklia wa Iran pamoja na biashara ya Kimataifa

USA Donald Trump und Emmanuel Macron im Weißen Haus in Washington
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Trump na Macron walikutana ana kwa ana kwa muda wa nusu saa kisha baadaye watakuwa na mkutano mkubwa zaidi wa saa nzima utakaohudhuriwa na wajumbe wengine, ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu nchini Marekani.

Rais Macron na mwenyeji wake Trump walijadili kwa kina juu ya hali ya kiuchumi ya Marekani, viwango vya uchumi vinavyokubalika, uchaguzi wa majimbo utakaofanyika mwezi Novemba nchini Marekani, udhibiti wa mitandao na mapambano dhidi ya ugaidi.

Rais wa Marekani Donald Trump, Emmanuel Macron wa Ufaransa pamoja na wake zao wakiwa ikulu ya white house MarekaniPicha: Reuters/C. Barria

Trump hana umaarufu sana nchini Ufaransa, lakini Macro kama viongozi wengine wa dunia, kwa mfano Shinzo Abe wa Japan na Theresa May wa Uingereza, wapo katika shinikizo la kuwaonesha wapiga kura umuhimu wa mahusiano mema na kiongozi huyo wa chama cha Republican aliye na miaka 71. Mazungumzo ya viongozi hao wawili pia yatagusia mkataba wa nyuklia wa Iran.

Aidha Rais Macron pamoja na mataifa mengine ya Ulaya yanapambana kuuokoa mkataba huo uliyo na utata wa nyuklia ya Iran ambapo Trump huenda akauweka pembeni atakapokataa kuondoa vikwazo  dhidi ya Iran ifikapo tarehe 12 Mei.

Rais wa Iran Hassan Rouhani asema nchi yake itajibu iwapo makubaliano ya nyuklia yatavunjwa.

Kwa upande wake Rais Hassan Rouhani wa Iran amemtaka mwenzake mwa Marekani, Donald Trump, kubakia ndani ya makubaliano ya nyuklia yaliyotiwa saini na mataifa yaliyo na nguvu duniani mwaka 2015 au wapambane na majibu makali. Rouhani amesema iwapo Trump atavunja makubaliano hayo, wako tayari kuanzisha tena mpango wake wa nyuklia ambao nchi za Magharibi zinahofia kwamba unaweza kutengeneza mabomu.

Amesema nchi yake iko tayari kupambana na hali yoyote ile. Tayari Trump alishaonya kwamba iwapo makosa katika mpango huo hayatarekebishwa ifikapo Mei 12, basi atarejesha tena vikwazo vya kiuchumi vilivyoekewa Iran, jambo ambalo litakuwa pigo kubwa dhidi ya mkataba huo.

Rais wa Iran Hassan RouhaniPicha: picture-alliance/AA/F. Bahrami

Mataifa yote yaliyotia saini mkataba huo - yaani Urusi, China, Ujerumani, Uingereza na Ufaransa - yanasema yangelipenda kuuendeleza mkataba huo huo uliosimamisha mpango wa Iran wa kutengeneza nyuklia baada ya vikwazo vya kiuchumi kuondolewa. Na ndio maana Rais Macron yupo nchini Marekani kwa ziara hiyo ya siku tatu kujaribu kumshawishi Trump kutoyavunja makubaliano.

Lakini kwa upande mwengine, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alisema hapo jana kwamba wamekubaliana pamoja na mwenzake wa China kwamba watajaribu kupinga uwezekano wowote wa Marekani kuyasambaratisha makubaliano hayo.

Muandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW