Rais Maduro wa Venezuela achaguliwa kwa muhula wa tatu
29 Julai 2024Tume ya uchaguzi imesema Maduro ameshinda kwa asilimia 51.2 ya kura. Rais wa Tume ya Uchaguzi ya CNE Elvis Amoroso, amewaambia waandishi habari kuwa asilimia 44.2 imekwenda kwa mgombea wa upinzani Edmundo Gonzalez.
Matokeo hayo yametangazwa katika wakati wapinzani wa Maduro walikuwa wanapanga kuyapinga.
Jana jioni wengi ya wanasiasa wa upinzani walikuwa wameanza kushangilia kupitia mitandao ya kijamii wakisema mwelekeo uliokuwa unaonesha mgombea wao Gonzalez angepata ushindi wa kishindo.
Matumaini yao yalitokana na uchunguzi wa maoni ya wapigakura kuonesha Gonzalez alikuwa akiongoza na alikuwa na nafasi nzuri ya kuibuka mshindi.
Tume ya uchaguzi ambayo inadhibitiwa na watu watiifu kwa Maduro bado haijachapisha matokeo yote kutoka vituo 30,000 vya kupigia kura.
Upinzani ulisema tangu mapema kwamba unatilia mashaka uhuru wa uchaguzi huo hasa baada ya wafanyakazi wake kadhaa kukamatwa.
Wawakilishi wa upinzani wanasema karatasi za majumuisho ya kura waliyokusanya kutoka kwa mawakala wao wa uchaguzi katika asilimia 30 ya vituo vya kupigia kura zinaonesha Gonzalez alikuwa amemshinda Maduro.
Katika uchaguzi huo wa jana, Maduro alipata upinzani mkali zaidi tangu alipoingia madarakani.
Mgombea wa upinzani Edmundo Gonzalez ambaye ni mwanadiplomasia wa zamani alikuwa na uungwaji mkono mkubwa ikiwemo kutoka kwa nyota wa upinzani Maria Corina Machado ambaye alizuiwa kugombea nafasi yoyote ya kisiasa mwaka jana.