1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Magufuli awaapisha mawaziri wapya

George Njogopa (DW Dar es Salaam)22 Julai 2019

Baada ya kutengua uteuzi wa waziri wa Mazingira nchini tanzania, January Makamba, rais John Magufuli, amewaapisha mawaziri wapya na kuwataka wafanye kazi kwa weledi.

Präsident John Magufuli aus Tansania
Picha: DW/S. Khamis

Kwa mara nyengine tena Rais John Magufuli wa Tanzania amewaapisha mawaziri wapya kwenye serikali yake, huku akibainisha sababu za kumfuta kazi aliyekuwa waziri wake wa Muungano na Mazingira, Januari Makamba, na pia za kumteuwa mkosoaji wake Hussein Bashe kuwa naibu waziri wa kilimo, lakini bado akiwacha maswali mengi zaidi kwenye utenguzi wa safari hii.

Rais Magufuli ambaye amekuwa akilipangua mara kwa mara baraza lake la mawaziri amesema wizara hiyo ya Muungano na Mazingira ilikuwa ikisuasua katika utekekezaji wa baadhi ya mambo. Ametolea mfano suala la upigaji marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki akisema kwamba licha ya kutaka jambo hilo lifanyike zaidi ya miaka minne iliyopita, lakini utekelezaji wake ulikuwa hadi hadi pale alipoamua kuingilia kati.

Januari Makamba alifutwa kazi jana na nafasi yake kuchukuliwa na George Simbachawene, ambaye amewahi pia kufutwa kazi na Rais Magufuli kabla ya kurejeshwa tena.

Rais Magufuli akisalimiana na naibu waziri mpya wa kilimo Hussein BashePicha: DW/S. Khamis

Tabia ya Rais Magufuli kutenguwa na kuteuwa wasaidizi wake imekuwa jambo la kawaida kiasi cha kwamba halishituwi tena, lakini kuondolewa kwa Makamba kumezua gumzo kubwa mitaani na mitandaoni, hasa kwa kuzingatia kuwa alikuwa akitajwatajwa kuwa ni miongoni mwa mawaziri wachapa kazi.

Miongoni mwa waliopaza sauti kukosoa utenguzi wa Makamba, ni kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ambaye mapema leo aliandika kupitia mitandao yake ya kijamii akipinga sababu zilizotajwa na Rais Magufuli kuwa sababu ya kumuondoa waziri huyo.

Hata hivyo, mwenyewe Makamba amesema amepokea kwa mikoni miwili uamuzi wa kuondolewa kwenye wadhifa huo na kueleza atasema mengi zaidi katika siku za usoni. Mrithi wake, Waziri Simbachawene ameahidi kuchapa kazi kwa weledi na maarifa ili kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye wizara hiyo.

Waziri ambaye uteuzi wake ulitenguliwa January MakambaPicha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Rais Magufuli amemwapisha pia mkosoaji mkubwa wa utendaji kazi wa serikali yake, Hussein Bashe, kuwa naibu waziri wa kilimo. Bashe ni mashuhuri kwa kuibana serikali wakati akiwa bungeni.

Rais Magufuli sasa amemtaka yale aliyokuwa akiyaonyesha bungeni ayaleta katika uhalisi wakati anapochukua jukumu jipya.

Rais Magufuli mara kwa mara amekuwa akiwaonya mawaziri wake kuwa hatasita kuwaondoa kwenye nyadhifa zao kama watashindwa kwenda na kasi ya utendaji wake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW