1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mnangagwa aahidi kufufua uchumi wa Zimbabwe

Sylvia Mwehozi
20 Desemba 2017

Rais mpya wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amesema suala la kufufua uchumi wa nchi hiyo ndio kipaumbele chake cha kwanza. Mnangangwa ameyasema hayo katika hotuba yake kuhusu hali ya taifa leo mjini Harare.

Emmerson Mnangagwa Simbabwe
Picha: picture-alliance/Zumapress/C.Yaqin

Rais Emmerson Mnangagwa amesema atazindua sera mpya na imara zitakazokuwa shirikishi na kufungua milango ya nchi hiyo katika uwekezaji wa kigeni, baada ya miaka kadhaa ya taifa hilo kutengwa. Mnangagwa alikuwa akihutubia taifa ikiwa ni hotuba yake ya kwanza tangu achukue madaraka mwezi uliopita baada ya kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe kujiuzulu. "Serikali hivi karibuni itazindua programu shirikishi na jumuiya ya kimataifa katika jitihada za kuungana na jumuiya ya mataifa mengine," amesema rais huyo.

Mnangagwa ameahidi kwamba hatovumilia vitendo vya rushwa katika jitihada za kufufua uchumi uliodhoofika, akisema ndio chanzo kikubwa cha matatizo yanayoikumba nchi hiyo. Chini ya Mugabe, Zimbabwe ambayo wakati mmoja iliwahi kuwa moja ya taifa imara kusini mwa Afrika, ilijikuta imetengwa wakati Marekani na mataifa mengine yaliopoiwekea vikwazo juu ya ukiukaji wa haki. Sheria zinazotishia kufungwa kwa biashara za kigeni ziliuweka kando uwekezaji.

Wafuasi wa Zimbabwe wakisherehekea kuapishwa kwa MnangagwaPicha: picture alliance/dpa/NurPhoto/B. Khaled

Rais huyo mpya amesema utawala wa Zimbabwe utawavutia wawekezaji. Mnangagwa ataitembelea Afrika Kusini hapo kesho kukutana na wawekezaji muhimu pamoja na rais jacob Zuma. Pia amewahimiza wafanyabiashara kudhibiti bei ya vyakula iliyoshuhudiwa katika wiki za hivi karibuni. Kuhusu uwekezaji, rais huyo anasema kwamba, "serikali yangu ina dhamira ya kuifungua Zimbabwe katika sekta ya uwekezaji kwa kutengeneza uchumi huru na ulio wa wazi , utakowanufaisha Wazimbabwe na kuwakaribisha watu wa nje."

Zimbabwe kwa hivi sasa inakabilliwa na uhaba mkubwa wa fedha na ukosefu mkubwa wa ajira ambao umewalazimisha mamilioni ya watu kuondoka nchini humo na wengine kugeukia biashara za mtaani.

Rais Emmerson Mnangagwa akiwaapisha mawaziriPicha: picture alliance/AP Photo/T. Mukwazhi

Wengi wakiwa wapinzani, ambao waliondolewa pia katika baraza la mawaziri wanamfuatilia kwa karibu Mnangagwa, mshirika wa siku nyingi wa Mugabe kuona kama ataleta mageuzi aliyoahidi. Rais huyo mpya amesema uchaguzi wa mwakani utakuwa wa kuaminika, huru na haki, ambapo Marekani na mataifa mengine yanahesabu kama hatua muhimu katika mageuzi.

Kufuatia ziara yake ya kwanza hapo kesho nje ya nchi kama rais, rais Mnangagwa anapaswa kuacha madaraka kwa msaidizi wake na ameahidi kwamba atachagua makamu wa rais wawili katika siku chache zijazo. Constantino Chiwenga aliyekuwa mkuu wa jeshi anapewa nafasi ya juu hali inayoonekana ni kulipa fadhila kwasababu ya kuongoza operesheni ya kijeshi iliyomgeuka Mugabe. Iwapo atateuliwa kuwa makamu wa Rais, itadhihirisha kuwa jeshi lina nafasi muhimu zaidi katika siasa za Zimbabwe.

Rais Mnangagwa ameteua maafisa kadhaa waandamizi wa jeshi katika baraz lake la mawaziri na katika chama tawala tangu alipoapishwa kuwa rais Novemba 24. Kamanda wa jeshi Phillip Sibanda atachukua mikoba ya Chiwenga kama mkuu wa majeshi, kwa mujibu wa taarifa ya serikali.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga