1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mnangagwa aapishwa tena baada ya miezi tisa madarakani

Oumilkheir Hamidou
26 Agosti 2018

Wazimbabwe wanasherehekea kuapisha rais Mnangwagwa kwa mhula wa pili katika kipindi cha miezi tisa katika wakati ambapo nchi hiyo inakabwa na mitihani mengine tangu ya upande wa upinzani mpaka mabishano ya uchaguzi.

Simbabwe Amtseinführung nach Präsidentenwahl
Picha: Reuters/P. Bulawayo

 

Rais anaeungwa mkono na jeshi, Emmerson Mnangagwa ameapishwa tena leo,  na mwanasheria mkuu Luke Malaba mbele ya umati wa watu  waliokusanyika katika uwanja wa taifa mjini Harare. Viongozi wa serikali kutoka Afrika Kusini, Congo, Rwanda Zambia na kwengineko wamehudhuria sherehe hizo. Rais Mnangagwa anakabiliwa na jukumu kubwa la kuijenga upya nchi hiyo iliyofilisika kiuchumi na kuliunganisha taifa linalokumbwa na mfarakano mkubwa kutokana na uchaguzi ambapo wengi walitaraji ungeleta mageuzi.

"Shauku si kubwa hivyo mjini Harare, ngome ya upande wa upinzani."Si rais wangu" nende kwanini" amesema mkaazi mmoja wa mji huo kwa jina Emmanuel Mazunda.

Kiongozi wa chama cha upinzani MDC Nelson ChamisaPicha: Getty Images/AFP/J. Njikizana

Wito wa suluhu wa rais Mnangagwa  haujaitikwa na kiongozi wa upinzani Chamisa

Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75 aliyetwaa madaraka kwa msaada wa jeshi dhidi ya mlezi wake wa kisiasa Mugabe Novemba mwaka jana alisema "mlango wake ni wazi na mikono anamnyoshea kiongozi wa upinzani Nelson Chamisa" , baada ya korti ya katiba kuyakataa ijumaa iliyopita madai ya upande wa upinzani dhidi ya visa vya udanganyifu na kumthibtisha kama mshindi wa uchaguzi wa Julai 30 iliyopita.

"Umewadia wakati wa kusonga mbele kwa pamoja" amesema Mnangagwa aliyeahidi mageuzi ya kidemokrasi na kiuchumi baada ya miaka 37 ya utawala wa Mugabe.

Chamisa amesema hautambui uamuzi wa korti ya katiba na kuzitaja sherehe za kuapishwa  kuwa ni "za uwongo."

"Wanajua hawawezi kunialika katika harusi ambayo mie ndie niliyekuwa nipokee zawadi, amesema. Msemaji wake, Nkululeko Sibanda amesema "hawakupokea mwaliko wowote rasmi kuhudhuria sherehe hizo."

Chamisa, mwenye umri wa miaka 40 ametoa wito wa kuzungumza na Mnangagwa lakini anasema mazungumzo ya kugawana madaraka yanabidi kwanza yamtambue kiongozi huyo wa upinzani kuwa ndie mshindi wa uchaguzi."Huwezi kuniibia mbuzi wangu na baadae unambie nije tugawane ."Anasema.

Wafuasi wa rais Mnangagwa washerehekea kuapishwa kwakePicha: Getty Images/AFP/Z. Auntony

Uchumi wa Zimbabwe uko ukingoni mwa muflisi

Msemaji wa chama tawala Paul Mangwana anamkosoa Chamisa kwa kukataa kushiriki katika sherehe za kuapishwa rais Mnangagwa."Ni muhimu katika wakati huu tete wa kulijenga taifa.Tatizo ni kwamba Vuguvugu la mageuzi ya kidemokrasi halikutupatia kiongozi  bora wa chama cha upinzani, wametupatia mwanafunzi anaecheza na sera za shule": Mangwana ameliambia shirika la habari la Associated Press.

 Uchumi wa Zimbabwe unalega lega. Wadadisi wanasema jukumu la haraka la Mnangagwa litabidi liwe kulipatia ufumbuzi tatizo la upungufu wa fedha taslimu na ukosefu ajira unaowalazimisha maelfu kugeuka wachuuzi majiani na wengine kuipa kisogo nchi hiyo.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP

Mhariri: Jacob Safari