Rais Mnangagwa ataweza kurejea madarakani?
23 Agosti 2023Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ni mpiganaji wa zamani wa msituni na mlinzi wa Robert Mugabe aliyejibu kufukuzwa kwake kazini kama makamu wa rais kwa kumuondoa madarakani kwa njia ya mapinduzi bosi wake Mugabe, mmoja wa viongozi waliotawala kwa muda mrefu zaidi duniani.
Mnangagwa sasa anawania kuchaguliwa kwa muhula wa pili kama rais wiki hii katika uchaguzi ambao huenda ukaongeza muda wa chama tawala ZANU-PF wa kukaa madarakani katika taifa hilo la kusini mwa Afrika ambalo linakabiliwa na vikwazo vya kimataifa. Chama hicho tawala kimekaa madarakani kwa miaka 43 sasa.
Zimbabwe imekuwa chini ya utawala wa ZANU-PF tangu mwaka 1980 ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa wazungu wachache.
Mnangagwa anayejulikana kwa jina la utani kama "mamba," jina hilo linaendana vizuri na mtu anayesifiwa na wafuasi wake kutokana na umahiri wake kisiasa japo kwa upande wa pili anakosolewa kwa kutokuwa na huruma.
Mnangagwa alimrithi Mugabe kama rais kufuatia mapinduzi ya kijeshi mwaka 2017, na alishinda uchaguzi uliozua utata mnamo mwaka 2018. Wakosoaji wake hata hivyo wanahisi kuwa ana chembechembe sawa na za mtangulizi wake Robert Mugabe. Hii ni licha ya ahadi alizotoa za kuwepo uhuru na demokrasia kwa raia milioni 15 wakati alipochukua usukani wa kuliongoza taifa.
Mugabe alikuwa ameiongoza Zimbabwe kwa miaka 37 na alionekana mzizi usiong'oleka. Kulingana na katiba, huu unapaswa kuwa muhula wa mwisho wa Mnangagwa iwapo atashinda uchaguzi wa Agosti 23.
Hata hivyo, baadhi ya wanachama kwenye chama chake wameeleza kuwa, sheria inapaswa kubadilishwa na kurudi jinsi ilivyokuwa enzi za Mugabe ili kumruhusu kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 80, kuendelea kusalia kama rais.
Mmoja wa wafuasi wake Rosedale Ndlovu amesema, "Tunamtaka atawale maisha yake yote.”
Mnangagwa mwenyewe amelikumbatia wazo hilo kwa mikono miwili, hivi karibuni aliliambia kundi moja la kidini na hapa namnukuu, "Ukitaka kuitawala nchi milele, njoo kanisani uombewe."
Hatarini ni mwelekeo wa taifa lenye utajiri wa madini na kilimo ambalo limeepukwa na mataifa ya Magharibi kwa zaidi ya miongo miwili kutokana na visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu. Badala yake, Zimbabwe imeigeukia China na Urusi kama washirika wake wa kiuchumi.
Muhula wa kwanza wa Mnangagwa: ZANU-PF yajinyakulia viti vingi bungeni Zimbabwe
Zimbabwe ina utajiri mkubwa wa madini ya Lithium barani Afrika na hivyo kuvutia maslahi kutoka China.
Mnangagwa ameahidi kuwaondoa raia wa taifa hilo kutoka minyororo ya ukandamizaji na kujitenga wakati wa enzi za Mugabe, japo kumekuwa na dalili ndogo tu ya mabadiliko.
Mashirika ya haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yameeleza kuwa ukandamizaji wa upinzani chini ya Mugabe aliyefariki dunia mwaka 2019 nchini Singapore, umeendelea pia chini ya utawala wa Mnangagwa. Mashirika hayo yametaja ukandamizaji huo kama "ukatili.”
Vikwazo vya Marekani na Ulaya bado vingalipo.
Baadhi wanahisi kuwa, sio jambo la kushangaza kwamba kumefanyika mabadiliko madogo mno hasa ukizingatia jinsi Mnangagwa alivyoingia madarakani, kwanza akiwa mlinzi wakati wa vita vya umwagaji damu vya uhuru katika miaka ya 1970, alafu kisha baadaye kuhudumu kama waziri katika miaka ya 80 na 90, na hatimaye kama makamu wa rais kabla ya usuhuba wao kuingia doa kiasi cha kufutwa kazi na Mugabe.
Mchambuzi wa kisiasa wa Zimbabwe Aleander Rusero amesema kabla ya Mugabe na Mnangagwa kutofautiana, Mnangagwa alichukuliwa kama mtiifu sana kwa Mugabe.
Amani: Wazimbabwe waombea amani wakati wa uchaguzi tete unakaribia
Wakati huu anapokalia kiti, kiongozi huyo anaonekana kuiga baadhi ya mitazamo ya Mugabe japo sio yote. Kwa mfano linapokuja suala la kuyakemea mataifa ya Magharibi, Mnangagwa anajaribu kupima maneno yake kwa tahadhari badala ya kuikaripia Ulaya kama alivyokuwa akifanya mtangulizi wake.
Alipoulizwa kuhusu jina lake la utani la mamba, Mnangagwa amejieleza kama mtu laini kama safu. Mara kwa mara, hutumia neno "hallelujah” wakati anapotoa hotuba zake katika taifa hilo la Kikristo.
Wakati wa kampeni, aliwambia wafuasi wake kuwa watakwenda mbinguni iwapo watakipigia kura chama chake. Anajipiga kifua kwamba Zimbabwe sasa imekomaa kidemokrasia chini ya utawala wake.
Aghalabu huonekana hadharani akiwa amevaa skafu yenye bendera ya Zimbabwe, akijionyesha kama mwokozi wa taifa.