1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Moon wa Korea Kusini yu tayari kukutana na Kim Jong-un

Daniel Gakuba
10 Januari 2018

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in amesema yu tayari kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un ikiwa masharti kadhaa yatatimizwa. Moon pia amesisitiza umuhimu wa suluhisho la mzozo wa nyuklia ya Korea Kaskazini.

Südkorea PK Moon Jae-in
Moon Jae-In, Rais wa Korea KusiniPicha: Reuters/Jung Yeon-Je

Rais Moon Jae-in ameelezea msimamo wake katika mkutano na waandishi wa habari ambao umeonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni. Kiongozi huyo wa Korea Kusini amesifu uamuzi wa Korea Kaskazini kutuma wanariadha wake kushiriki katika michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi itakayoanza mwezi ujao katika mji wa Pyeongchang nchini Korea Kusini, akisema kushiriki kwa Wakorea Kaskazini ni kitu walichokihitaji sana.

Rais wa kamati ya kimataifa ya michezo ya Olimpiki Thomas Bach pia amekaribisha kushiriki kwa wanariadha wa Korea Kaskazini, akisema ni hatua nzuri kwa maana na malengo ya michezo ya Olimpiki.

Hata hivyo Rais Moon ametilia mkazo suluhisho la mzozo juu ya mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini kama njia pekee ya kuleta amani kwenye rasi ya Korea.

''Kwa wakati huu tunapaswa kuileta Korea ya Kaskazini katika majadiliano ya kuondoa silaha za nyuklia na pia juu ya namna ya kuboresha mahusiano baina ya nchi mbili'', amesema Rais Moon, na kuongeza kuwa ni kwa masharti hayo tu ambapo atazungumzia kufungua tena eneo la viwanda la Kaesong, na safari za watalii kuzuru mlima wa Kumgang.

Mtazamo tofauti na Marekani

Moon, mliberali anayependelea suluhisho la kidiplomasia kuhusu mzozo wa nyuklia wa Korea Kaskazini, amesema yeye ataacha mlango wazi, ikiwa pamoja na uwzekano wa mazungumzo ya ana kwa ana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, lakini tu ikiwa mazungumzo hayo yataleta maelewano baina ya Korea mbili, na kuondoa mvutano kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Mazungumzo ya jana baina ya Korea mbili yalileta matumaini ya kupunguza mvutanoPicha: IANS

Mtazamo wake wa maridhiano unatofautiana na ule wa Marekani ambaye ni mshirika wa karibu wa Korea Kusini, ambayo inashikilia kuwa sharti Korea Kaskazini iache kufanya majaribio ya silaha za nyuklia kabla ya kufanyika kwa majadiliano yoyote.

Rais wa Korea Kusini amejaribu kupuuza tofauti hiyo ya maoni kati yake na Marekani, akisema Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia ni kitisho kwa nchi zote mbili.

Korea ya Kaskazini yasema mpango wao wa nyuklia haujadiliwi

Katika mkutano uliofanyika jana baina ya maafisa wa ngazi ya juu wa Korea mbili, kiongozi wa ujumbe wa Korea Kaskazini alisisitiza kuwa mpango wa nyuklia wa nchi yake hauwezi kuwa katika agenda ya mazungumzo, na kwamba hatua yoyote ya kutaka uzungumziwe itaathiri nia njema kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini.

Akijibu swali la iwapo mbinyo wa Rais Trump umeilazimisha Korea Kaskazini kuridhia wito wa mazungumzo, Rais Moon Jae-in amesema bila shaka hilo limechangia. Vile vile ametaka vikwazo vizidi kuimarishwa dhidi ya jirani wake wa Kaskazini, akiahidi kubakisha pale pale vikwazo binafsi ambavyo Korea Kusini imeiwekea Kaskazini hadi pale nchi hiyo itakapokubali mazungumzo juu ya silaha zake za nyuklia na makombora.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, dpae

Mhariri: Caro Robi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW