Rais Mpya wa Afrika Kusini kuidhinishwa alhamisi
25 Septemba 2008Bunge la Afrika Kusini linatarajiwa kumuidhinisha makamu mkuu wa chama tawala cha African National Congress ANC Kgalema Motlanthe kama rais wa muda wa taifa ambalo linaonekana limezongwa na mgogoro mkali wa kisiasa tangu kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi.
Hatua ya kumuidhinisha Kgalema Motlanthe kama rais wa Afrika Kusini inafuatia kuteuliwa kwake mapema wiki hii baada ya rais Thabo Mbeki kujiuzulu mwishoni mwa juma kutokana na kuombwa kufanya hivyo na uongozi wa chama chake cha ANC.
Motlanthe,msomi na mwenye mwelekeo wa kushoto,tena mshirika mkuu wa Zuma, anaheshimiwa sana sio tu na wafuasi wa mrengo wa kushoto lakini pia na jamii ya wafanya biashara wa ANC.
Ni mwanafunzi wa zamani aliekuwa mkereketwa pamoja na mwana chama cha wafanya kazi.Anaonekana kama mtu anayeweza kusaidia kuziba mgawanyiko ulioko ndani ya chama pamoja na kutuliza wasiwasi nchini humo.
Mgawanyiko ndani ya chama pamoja na wasiwasi vilijitokeza kufutia kujizulu kwa Bw Mbeki mwishoni mwa juma.
Kufutia kujiuzulu huko karibu theluthi mbili ya baraza lote la mawaziri ilijiuzulu siku ya jumanne kutokana na utiifu wao kwa Bw Mbeki.
Mtafaruko huo wa kisiasa umezusha wasiwasi kuwa huenda mgawanyiko zaidi katika chama hicho ukatokea.
Pia habari zaidi kutoka Afrika kusini zinasema kuwa Mbeki mwenyewe hatahudhuria sherehe za alhamisi japo alipewa mwaliko.
Kuondoka kwa Bw Mbeki ndio kilele cha mvutano mrefu na mkali na Zuma aliempiku katika nafasi ya kiongozi wa chama cha ANC katika uchaguzi uliofanyika Disemba.
Mvutano wao umevuruga malengo ya chama hicho na kukifanya kusahau masuala nyeti kama vile umaskini uliokithiri,pamoja na janga la UKIMWI linalowakabili raia mamilioni kadhaa nchini humo.
Aidha kuondoka kwa Mbeki pia kunaonekana kumepokelewa kwa maoni tofauti nje ya Afrika Kusini.
Katika nchi jirani ya Zimbabwe, rais wake Robert Mugabe inasemekana amekuchukulia kama pigo.
Kwa mujibu wa gazeti la serikali la The Herald,likimnukuu Mugabe akiwaambia maripota mjini New York-Marekani, anakohudhuria mkutano wa baraza la Umoja wa Mataifa kuwa,ingawa si habari njema lakini hatua hiyo imeamuliwa na watu wa Afrika Kusini.
Mbeki, licha ya kulaumiwa mwanzo kwa njia yake ya kumdekeza Mugabe katika mgogoro wa Zimbabwe, lakini mapema mwezi huu alifanikiwa kufanikisha mpango wa kugawana madaraka kati ya mahasimu wawili wa mjini Harare.
Na rais Mugebe anasemekana kusema kuwa licha ya yaliyomfika rafiki yake Mbeki, lakini yuko tayari kushirikiana na upinzani nchini mwake Zimbabwe katika kugawana madaraka.
Nacho chama cha upinzani nchini Zimbabwe cha Morgen Tsvangirai cha Movement for Democratic Change kinasema hakitarajiii kuwa kujiuzulu kwa Mbeki kutaathiri majadiliano yanayoendelea kati yake na chama cha Mugabe cha ZANU PF.
Katika mpango uliofanikishwa na Mbeki wa kugawana madaraka,Tsvangirai aliteuliwa kama waziri mkuu.