1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya wa Malawi aapa kukabiliana na ufisadi

4 Oktoba 2025

Rais mpya wa Malawi, Peter Mutharika, amechukuwa rasmi madaraka leo Jumamosi na kutoa ahadi ya kukomesha ufisadi uliokithiri pamoja na kufufua uchumi wa taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Malawi Goliati 2025 | Rais Mutharika
Rais mpya wa Malawi, Peter Mutharika (katikati)Picha: Joseph Mizere/Xinhua/picture alliance

Maelfu ya wafuasi, wakiwa wamevalia mavazi ya kitamaduni ya buluu ya chama cha Mutharika cha Democratic Progressive Party, walijaa kwenye uwanja wa Kamuzu katika mji mkuu wa kibiashara wa nchi hiyo, Blantyre kushuhudia kuapishwa kwa rais huyo.

Akihutubia umati huo, Mutharika amesema wamerejea na maono mapya na ajenda mpya.

Ameongeza kusema kuanzia leo rushwa imekwisha na akaonya kuwachukulia hatua waporaji wa serikali.

Chakwera hakuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa Mutharika

Rais anayeondoka Lazarus Chakwera, hakuhudhuria sherehe hiyo ya leo. Chama chake kimesema jina lake liliondolewa kwenye orodha ya wageni waalikwa katika dakika za mwisho.

Chama hicho pia kimesema Chakwera alikuwa amejitolea kuhudhuria binafsi hafla hiyo na kupokeza madaraka katika tukio hilo la kihistoria, lakini kinaheshimu uamuzi wa kumuacha nje ya hafla hiyo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW