Rais mpya wa Pakistan kuteuliwa na wabunge Jumamosi
6 Septemba 2008Aliewekewa matumaini makubwa ya kuchaguliwa ni Asif Ali Zardari,kiongozi wa chama cha Pakistan People´s Party PPP. Wapinzani wake ni Jaji Mkuu Saeed-Zu-Zaman Siddiq anaeungwa mkono na Waziri Mkuu wa zamani Nawaz Sharif na mwengine ni Mushahid Hussain alie mshirika wa karibu wa Musharraf.
Hapo zamani Asif Ali Zardari alikuwa akiitwa "Bwana asilimia kumi" miongoni mwa Wapakistani wa kawaida na hata nje ya nchi kwa jinsi sifa yake ilivyochafuka kwa tuhuma za rushwa.Lakini mivutano ya kisiasa na mashtaka ya mahakama yaliyomtia jela miaka 11 mume wa waziri mkuu wa zamani,hayati Benazir Bhutto,hayatoathiri uchaguzi wa rais.Vile vile mwaka jana alisamehewa mashtaka mengine.
Inatazamiwa kuwa kura zitakazopigwa kwa siri na mabunge mawili na mabaraza manne ya wilayani,zitamuunga mkono Zardari kuchukua nafasi ya Pervez Musharraf alieshinikizwa kujiuzulu mwezi uliopita.Lakini miongoni mwa raia wapatao milioni 160 katika dola lenye nguvu za nyuklia,kuna wasi wasi iwapo Zardari anafaa kupewa madaraka yatakayomruhusu kuvunja serikali na kuchagua viongozi wa jeshi la taifa lenye nguvu kubwa.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Shafqat Mahmood aliewahi kuwa mbunge anasema,wengi wanaamini kuwa sifa ya Zardari imechafuka kwa tuhuma za rushwa,dhuluma na mauaji.Wanahisi hali kama hiyo ni kizuizi kikubwa kwa mgombea cheo chenye madaraka makubwa kabisa nchini humo.Isitoshe,Zardari mwenye miaka 52 hajakubali kuwa yeye kwa sehemu kubwa,ndio aliesababisha maafa yaliyomkuta mkewe kama waziri mkuu.Daima ameshikilia kuwa mashtaka dhidi yake yalichochewa kisiasa na hakuna kilichothibitishwa.
Kwa kweli si wengi waliomfahamu Zardari alipomuoa Bhutto katika mwaka 1987,lakini mara alijipatia cheo chenye madaraka kama waziri serikalini, akivutiwa zaidi na sekta za uchumi na mazingira.Yeye alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutiwa ndani,serikali za mkewe zilipoondoshwa madarakani.Mara ya kwanza katika mwaka 1990 alikuwa jela miaka mitatu kabla ya kurejea katika serikali ya pili ya Benazir Bhutto.Lakini mwaka 1996 alirejeshwa tena jela baada tu ya serikali hiyo kuondoshwa madarakani. Zardari alikuwa jela miaka minane kabla ya kufunguliwa Novemba 2004 baada ya kutokutikana na hatia katika mashtaka ya mwisho kutoka jumla ya mashtaka 17.
Kifo cha Benazir Bhutto Desemba mwaka jana,kilimrejesha Zardari katika uwanja wa kisiasa.Baada ya kutengwa kwa miaka kadhaa na PPP kilichoongozwa na mkewe,Zardari alishika usukani wa chama hicho na sasa anakiongoza katika serikali ya mseto iliyo dhaifu.Uteuzi wake umekubaliwa kwa wingi mkubwa na PPP lakini kinasema,idhini hiyo kwa sehemu fulani imetolewa kwa heshima ya Bhutto aliejitolea muhanga.Lakini maisha ya zamani ya Zardari huenda yakawa tatizo kwa Pakistan.