Rais mteule wa Burundi atoa ahadi ya mwanzo mpya
26 Mei 2020Akihutubia baada ya kutangazwa mshindi Ndayishimiye amesema ushindi wake ni wa raia wote waliomchagua na wale ambao hawakumchagua.
Hivyo hakuna sababu ya wafuasi wa chama kimoja kuwabugudhi wengine. Pia ameitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono hatua iliyofikiwa nchini humo.
Kiongozi hiyo wa chama cha CNDD-FDD aliyeibuka mshindi uchaguzi wa Mei 20 ameongeza kusema kuwa uchaguzi huu umedhihirisha kukuwa kwa umahiri wa kisiasa wa Burundi. Ndayishimiye ameahidi kuwasikiliza raia wote Burundi bila ubaguzi.
''Tumejipa hadhi mbele ya Warundi na dunia, kwa kuionesha kuwa tulipofikia hatufundishwi tena demokrasia bali tunaweza kuwafundisha wengine. Hivyo ninaahidi kuwa nitawasikiliza wananchi wote bila ubaguzi ili maoni yao yaweze kulijenga taifa. Hivyo naitaka jumuia ya kimataifa kuiunga mkono hatua hii ya kupendeza tuliyoifikia''. amesema Ndayishimiye
Pia Ndayishimiye amemshukuru mtangulizi wake Rais Pierre Nkurunziza kwa hatua yake ya kuridhia alivyoridhia kuanzisha mchakato huu wa uchaguzi. Ndayishimiye amewataka wakimbizi kurudi nyumbani kuchagina katika ujenzi wa taifa.
Upinzani wapinga ushindi wa Ndayishimiye
Naye Agathon Rwasa aliyechukua nafasi ya pili, kwa kupata asilimia 24 ya kura, amesema hatokubaliana na matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Rwanda, CENI.
Rwasa ameahidi kuyafikisha malalamiko yake kwenye mahakama ya kikatiba na endapo hatotendewa haki basi ataelekea kwenye mahakama ya Jumuia ya Afrika Mashariki.
Tayari tume ya Uchaguzi inakutana na wawakilishi wa vyama vya siasa ili kuwateuwa wabunge 21 kutoka katika jamii ya Watutsi na Watwa 3 watakaojumuishwa katika bunge la taifa ili kuleta usawa wa kikabila.
Ndayishimiye ni nani lakini?
Ndayishimiye aliyehudumu kama jenerali katika jeshi, amekuwa katibu wa chama tawala cha CNDD-FDD tangu mwkaa 2016. Kabla ya kuchaguliwa kuwa rais, alikuwa mkuu wa idara ya masuala ya kijeshi chini ya afisi ya rais Pierre Nkurunzinza.
Ndayishimiye pia alihudumu kama waziri wa masuala ya ndani katika kipindi cha mwaka 2006-2007.
Ndayishimiye anayefahamika kwa jina la utani kama ''Neva'' alihudumu katika jeshi kwa muda mrefu kabla ya kujiunga katika siasa. Alikuwa mwanafunzi mdogo katika chuo kikuu cha Burundi mwanzoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwaka 1993.
Marafiki wa Ndayishimiye, wanamtaja kuwa mtu mwenye fikra huru lakini wakati huo huo mwenye hasira za haraka. Mmoja wa marafiki zake anasema Ndayishimiye ni mtu wa matani mengi na hupenda sana kucheka.
Mjumbe mmoja naye amesema kuwa rais huyo mpya ameonesha uwazi na uaminifu tofauti na majenerali wengine lakini atakabiliwa na wakati mgumu atakapoanza kutekeleza majukumu yake.
Tofauti na Nkurunziza ambaye wengi wamemtaja kuwa mtu katili, Ndayishimiye hajahusishwa na dhulma za hivi karibuni zilizofanywa na chama cha CNDD-FDD dhidi ya wale wanaoonekana kuwa wakosoaji. Hata hivyo hakuingilia kati kutuliza ghasia zilizolikumba taifa hilo kufuatia uchaguzi uliokumbwa na utata wa mwaka 2015.