Rais mpya wa Iran asema hatakutana na Rais Joe Biden
21 Juni 2021Rais huyo mteule wa Iran Ibrahim Raisi amewaambia waandishi wa habari kwamba Marekani inapaswa kuondoa vikwazo kandamizi vyote dhidi ya Iran. Juu ya mpango wa nchi yake wa makombora ya masafa marefu kiongozi huyo anayezingatiwa kuwa mwenye msimamo mkali, amesema suala hilo pamoja na la kuwaunga mkono wanamgambo katika ukanda wa mashariki ya kati si ya kuzungumziwa.
Marekani haijajibu kauli ya rais wa Iran. Alipoulizwa juu ya uwezekano wa kukutana na rais Joe Biden, rais mteule wa Iran alijibu kwa kifupi kwa kusema hapana! Amesema Marekani kwanza itapaswa kuondoa vikwazo vya kiuchumi ili kuonyesha iwapo inaaminika. Ameeleza kuwa Marekani imeupuuza mkataba wa nyuklia kwa kuiewekea Iran vikwazo alivyoviita kuwa si ubinadamu hata kidogo. Baada ya wiki kadhaa za mazungumzo juu ya kuurejesha mkataba huo, bado hakuna dalili za kusonga mbele. Rais wa hapo awali Donald Trump aliiondoa Marekani kwenye mkataba huo mnamo mwaka 2018.
Rais mteule Ibrahim Raisi atakuwa rais wa kwanza wa Iran aliyemo madarakani ambaye amewekewa vikwazo na serikali ya Marekani hata kabla ya kuapishwa kuwa rais. Rais huyo mpya alikuwa kiongozi wa mahakama iliyoshutumiwa duniani kote kwa kuwamo miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kutoa adhabu ya kifo. Kwa upande mwingine ushindi wa bwana Raisi katika uchaguzi wa Iran umesababisha wasiwasi kwamba huenda ukatatiza njia ya kurejea kwenye mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015.
Kwenye mkutano na waandishi habari Rais Ibrahim Raisi pia alizungumzia juu ya uhusiano wa nchi yake na Saudi Arabia katika muktadha wa mazungumzo ya faragha yanayoendelea mjini Baghdad juu ya kupunguza mvutano baina ya nchi hizo mbili. Bwana Raisi amesema hana tatizo juu ya uwezekano wa kila upande kumrejesha balozi wake na kwamba hakuna vizingiti katika kurejesha uhusiano baina yao.
Vyanzo:/DPA/AP