Rais Mursi aitisha mjadala wa kitaifa
7 Desemba 2012Akihutubia taifa baada ya siku kadhaa za vurugu, Mohammad Mursi aliitisha mkutano wa mjadala wa kitaifa siku ya Jumamosi. Lakini hakutakuwa na kucheleweshwa kwa kura ya maoni juu ya katiba mpya ambayo imesababisha hasira kubwa miongoni mwa wapinzani wake. Mursi aliahidi kuwa madaraka yake mapya aliyojipa wiki mbili zilizopita yatafutika baada ya kura ya maoni ya Desemba 15 ikiwa katiba hiyo itapitishwa ama la.
"Haya yote yamepekelea mwaliko wa wazi kwa ajili ya mazungumzo, mwaliko niliyoutuma kwa viongozi wote wa kisiasa, vijana wa mapinduzi, wataalamu wa sheria na majaji ili wakutane kwa pamoja Jumamosi tarehe 8 Desemba 2012," alisema Mursi.
Rais Mursi atoa tahfifu za kisiasa
Awali rais Mursi alisema chaguo lililoko mbele ya wamisri ni kuidhinisha katiba mpya au kumuacha aendelee kuhodhi madaraka yake yasiyo na kifani, ambayo yanazifanya amri zake kuwa juu ya mamlaka ya mahakama. Mursi alisema yuko tayari kufuta kipengele katika tamko lake la kikatiba kinachomuwezesha kuchukua hatua hatua yoyote aliyoiona inafaa kulinda nchi na malengo ya mapinduzi.
Kufutwa kwa kura ya maoni kuhusu katiba limekuwa moja ya matakwa muhimu ya wapinzani, lakini badala yake, Mursi amesema mkutano wa Jumamosi utawashirikisha viongozi wa kisiasa na vijana katika majadiliano mapana na yenye ufanisi. Tahfifu za kisiasa alizokuwa ametoa Mursi, kwa wengi zilifunikwa na sauti ya ukali aliyotumia katika utangulizi wa hotuba yake, akisema kuwa demokrasia inamaanisha kuwa wachache laazima wakubaliane na matakwa ya wengi.
Moja wa viongozi wakuu wa upinzani Mohammed EL-Baradei ameelezea kusikitishwa kwake na hotuba ya rais Mursi. "Tulitarajia kuwa rais ataitikia wito wa kufuta tamko la kikatiba na kuchelewesha kura ya maoni hadi kuwepo na makubaliano ya kitaifa juu ya katiba. Tulitaka rais aitishe mjadala wa kitaifa kuinusuru nchi na mgawananiko unaoitishia."
Awalaumu wapinzani kwa uchochezi
Alisema watu 80 walikamatwa kufuatia vurugu za Jumatano mbele ya ikulu ya nchi hiyo, ambapo watu sita waliuawa, na kusema kinachosikitisha ni kuwa badhi ya waliokamatwa wanahusishwa na wale wanaojitambulisha kuwa viongozi wa kisiasa, ambao alisema wanatumia fedha zao walizozipata kwa njia za rushwa katika utawala uliyopita, kuifanyia ugaidi nchi.
Licha ya tahfifu zake, hotuba hiyo ilizusha hasira zaidi katika mitaa ya Cairo, ambapo waandamanaji walikuwa wanarushwa viatu nje ya ikulu katika ishara ya kupingana na ye. Waandamanaji pia walivamia na kuchoma moto makao makuu ya chama cha Udugu wa Kiislamu katika wilaya ya Moqattam mashariki mwa mji wa Cairo.
Rais wa Marekani Barack Obama alimpgia simu rais Mursi jana na kuelezea wasi wasi wake juu ya vifo na kujeruhiwa kwa waandamanaji. Obama alikaribisha hatua ya Mursi ya kuitisha mjadala wa kitaifa, lakini alisisitiza kuwa majadiliano hayo yafanyike bila kuwekeana masharti. Marekani imewashinikiza pia wapinzani kufanya hivyo.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae
Mhariri: Saum Yusuf