Rais Mwinyi atimiza siku 100 madarakani
8 Februari 2021Rais wa Zanzibar, Dokta Hussen Ali Mwinyi amesema hana wasiwasi wowote kuhusu majaliwa ya serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa hivi karibuni baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu ambao ulilalamikiwa na vyama vya upinzani.
Katika mahojiano maalum aliyofanya na DW Kiswahili Visiwani humo, rais Mwinyi ambaye leo anatimiza siku 100 madarakani, amedokeza matamanio yake kuhusu mwelekeo mpya wa kisiasa katika visiwa vya Zanzibar hasa baada ya kuundwa kwa serikali mpya ya Umoja wa Kitaifa inayovishirikisha vyama vya CCM na ACT-Wazalendo.
Soma Zaidi: Hussein Mwinyi na Maalim Seif wakutana na rais Magufuli kijijini Chato
Amenukuliwa akisema "Sina shaka na hilo kwa sababu serikali ya kitaifa ni suala la kikatiba, si hiyari ya mtu na sisi site tumaeapa kuilinda katiba. Kwa hiyo mimi sina shaka yoyote kwa sababu kwa kuwa jambo hili liko kwenye katiba yetu, yoyote aliyeko madarakani atalazimika kuifuata katiba kuunda serikali ya kitaifa endapo tutakuwa tumepata zile asilimia zinazokubalika kisheria za vyama hivi vinavyoingia katika uchaguzi."
Kwa miaka mingi Zanzibar imekuwa ikitawaliwa na hali ya sintofahamu ya kisiasa na visa vingi vya uhasama vimekuwa vikiibuka wakati na baada ya uchaguzi mkuu. Katika uchaguzi uliopita, chama cha ACT Wazalendo kilieleza kutoridhishwa kwake na mwenendo wa uchaguzi huu na kutupia lawama baadhi ya vyombo vya dola kwa kuwakamata wanachama wake.
Hii siyo mara ya kwanza kwa visiwa hivyo kuwa na serikali ya Umoja wa Kiataifa, lakini Rais Mwinyi amesisitiza kuwa hana shaka yoyote kuhusu majaliwa na umoja huo. Mbali na hilo Rais Mwinyi ameonya kuhusu wafanyakazi wazembe na wabadhilifu wa mali ya umma akisema mkono wake hautosita kuwashukia. Ameeleza shabaha ya serikali yake ni kuhakikisha anaitoa Zanzibar pale ilipo ni kuipeleka kwenye hatua itayotoa sura mpya ya kimaendeleo.
Kama ilivyo kwa utawala wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli, rais huyo wa Zanzibar amekuwa akichukua hatua za haraka ikiwamo kuwasimamisha kazi baadhi ya maofisa wa serikali na watumishi wa umma wanaotuhumiwa kwa kashfa za rushwa na kasi ndogo ya utendaji.
Serikali yake imefungua milango kwa wawekezaji wa kigeni na tayari imetiliana saini na Oman kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya kisasa. Wananchi visiwani Zanzibar wamekuwa na mitazamo ya aina mbalimbali kuhusu utendaji wake wa awali, wengi wakitumaini kufika mbali kwa visiwa hivyo.
Hata hivyo, Rais Mwinyi amekiri kuzorota kwa biashara ya utalii katika visiwa Zanzibar kulikotokana na janga la virusi vya corona linaloendelea kuisumbua dunia kwa sasa.
George Njogopa- Zanzibar.