1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ndayishimiye ana jukumu la kuleta mageuzi Burundi

18 Juni 2020

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limesema kuapishwa kwa Evariste Ndayishimiye kuwa rais mpya wa Burundi ni fursa ya kurejesha heshima kwa haki za binaadamu katika nchi hiyo

Neuer Präsident von Burundi, Evariste Ndayishimiye
Picha: DW/A. Niragira

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limesema kuapishwa kwa Evariste Ndayishimiye kuwa rais mpya wa Burundi ni fursa ya kurejesha heshima kwa haki za binaadamu katika nchi hiyo kwa kufungua upya nafasi za mashirika ya kiraia, kukomesha uhalifu unaofanywa chini ya sheria za kimataifa na ukiukiaji wa haki za binaadamu unaofanywa na vikosi vya usalama na tawi la vijana la chama tawala.

Amnesty international inamuhimiza Rais Ndayishimiye kuwaachia mara moja na bila masharti wale wote waliofungwa kwa makosa ya kutumia haki zao za binaadamu akiwemo Germain Rukuki, mtetezi wa haki za binaadamu anayetumikia kifungo cha miaka 32 jela kwa kazi yake na shirika moja linalopinga mateso.

Deprose Muchena ni Mkurugenzi Mkuu wa Amnesty International wa kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Serikali ya Nkurunziza inatuhumiwa kwa ukiukaji wa hakiPicha: Reuters/C. Guy Siboniyo

Wengine waliotiwa ndani kwa kutumia uhuru wa habari ni wanahabari wanne, Agnès Ndirubusa, Christine Kamikazi, Egide Harerimana na Térence Mpozenzi, ambao mnamo Januari 30 walihukumiwa kifungo cha miaka miwili na nusu jela na kutozwa faini ya dola za kimarekani 525 kila mmoja. Wote walilifanyia kazi shirika la Iwacu Press Group, mojawapo ya vyombo huru vichache vya habari vilivyobaki Burundi. Waliadhibiwa kwa kujaribu kuripoti kuhusu makabiliano makali yaliyozuka kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Amnesty International inatoa wito wa kuwachiwa kwao mara moja na bila masharti. Aidha shirika hilo linaitaka serikali kueleza aliko na hatima ya mwanahabari mwingine wa Iwacu, Jean Bagirimana, ambaye alitoweka tangu Julai 2016.

Tawi la vijana la chama tawala cha CNDD-FDD, Imbonerakure, linafahamika kwa kufanya ukiukaji wa wazi wa haki za binaadamu, ikiwemo mauaji, ukamataji wa kiholela, vipigo, na kuwasumbua watu kupitia uchokozi, kuwatisha na unyang'anyi. 

Kiongozi wa upinzani Agathon RwasaPicha: DW/A. Niragira

Shirika hilo linasema serikali inapaswa kuanza kwa kufanya uchunguzi wa haraka, usioegemea upande wowote, wa huru na wazi wa uhalifu chini ya sheria za kimataifa na ukiukaji wa haki za binaadamu ambao umeharibu maisha ya watu wasio na idadi na kuwalazimisha maelfu kwa maelfu ya wengine kuikimbia nchi hiyo.

Maafisa wa vikosi vya usalama vilivyo rasmi na visivyo rasmi wanaotuhumiwa kwa kuhusika na ukiukaji wa aina hiyo lazima wawajibishwe. Maafisa wa serikali walioamuru au kuruhusu uhalifu wa aina hiyo wanapaswa kuwachiwa kazi wakisubiri uchunguzi, na kukiwa na ushahidi wa kutosha, washitakiwe kwa njia ya haki katika mahakama za kawaida za kiraia.

Kwa miaka kadhaa, serikali ya Burundi imechukua mbinu ya kujitenga zaidi kwenye jukwaa la kimataifa. Rais Ndayishimiye anapaswa kuyashirikisha upya mashirika ya kiserikali katika kanda hiyo na jumuia ya kimataifa. Miongoni mwa mambo ya faida nyingine za haki za binaadamu, hiyo itahakikisha kuwa maafisa nchini Burundi wanapata vifaa vya kupambana na janga la COVID-19.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW