Rais Ndayishimiye azungumzia utawala bora Burundi
29 Desemba 2021Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye ameongoza kipindi cha kujibu moja kwa moja maswali ya waandishi habari na raia wa kawaida. Maswali kuhusu sheria na utawala bora ndio hasa yametawala kipindi hicho ambapo Rais Ndayishimiye amebaini azma yake ya kuona Warundi wakibadili mwenendo na kusisitiza juu ya umuhimu wa kuheshimu sheria. Amida ISSA na taarifa zaidi kutoka Bujumbura.
Rais Ndayishimiye alisisitiza kusema kuwa hakuna aliye juu ya sheria, baada ya raia wengi na waandishi habari kumuuliza maswali juu ya ukiukaji wa sheria, kubomolewa kwa nyumba, huku maswali mengine yakionekana kuogopwa.
Waandishi hao pia waliuliza maswali kuhusu madai ya mfanyakazi ya idara ya ujasusi kumuua raia aliyekuwa kizuizini, pamoja na baadhi ya viongozi wanaotajwa kuwa vigogo wakihusishwa na kuweka pingamizi katika utekelezwaji wa hukumu za mahakamani.
Rais Ndayishimiye aliongeza kusema kuwa wale wasiokuwa tayari kuikumbatia azma yake hiyo ya kupiga vita rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma, na kuwajibika katika majukumu waliokabiodhiwa wako huru kuacha kazi ili waletwe watakaokubaliana na nia yake hiyo. ''Mimi nilijipa nia ya kuona Burundi ikibadilika, kwa kuwa Burundi yenye viongozi waadilifu, wasiokuwa tayari kukubaliana na nia hiyo wako huru kuacha kazi ili waletwe wengine.'' Amesema Rais Ndayishimiye.
Pia amesema hapendelei kuona maafisa wanaoketi ofisini, bila ya kuingia mitaafani kuwafuatilia wafanyakazi. Pia hataki kuona maafisa wanaonunuwa magari ya kifahari ya bei ghali, kwa kutumia pesa ya serikali.
Rais amesema Burundi inazo rasilimali nyingi zinazoweza kuiendeleza nchi, yapo madini ya dhahabu, Coltan miongoni mwa madini mengine na kwamba yamekuwa yakiuzwa nje ya nchi.
Rais Ndayishimiye amefafanua kuwa kinachohitajika kwa sasa ni kuwepo na wataalam, na amekosoa kuona bado kuna Warundi waliobobea katika taaluma mbalimbali ambao wamesalia nje ya nchi.
Akijibu swali kuhusu wanasiasa waliokimbilia nje ya nchi na walio korokoroni endapo kuna uwezekano wa kuwapatia msamaha, Rais Ndayishimiye amesema kunahitajika kwanza kuchunguza vizuri, kama kweli wanasiasa hao wamebadilika ili kuepusha wasirudi kutenda makosa waliyoyatenda awali.
Rais Evariste Ndayishimiye amesema ripoti ya tume ya ukweli na maridhiano kuhusiana na mauwaji ya 1972, itakabidhiwa kwa wanasheria ili waweze kutathmini ni uovu upi uliotendeka. Huku akisema utawala wa zama hizo ulitekeleza ukatili mkubwa dhidi ya raia.
Kipindi cha Rais Ndayishimiye kujibu moja kwa moja maswali ya waandishi habari na raia wa kawaida ni mara ya kwanza kufanyika mjini Bujumbura.
Amida ISSA, DW BUJUMBURA