1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGuinea

Guinea ya Ikweta yaingia kwenye uchaguzi Jumapili

Saumu Mwasimba
18 Novemba 2022

Kuna chama kimoja tu cha upinzani kilichoruhusiwa katika siasa nchini Guinea ya Ikweta na rais Teodoro aliyekaa madarakani miaka 43 atarajiwa kuchaguliwa tena

Äquatorialguinea | Präsident Teodoro Obiang Nguema Mbasogo
Picha: Steeve Jordan/AFP/Getty Images

Wananchi wa Guinea ya Ikweta Jumapili wanateremka vituoni kupiga kura katika uchaguzi wa rais na rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo aliyeitawala nchi hiyo tangu Agosti mwaka 1979 anatarajiwa kushinda muhula wa sita katika uchaguzi huo.

Utawala wa kiongozi huyo unajulikana kwa ukandamizaji wa wapinzani na kushuhudia majaribio kadhaa ya mapinduzi.

Nguema mwenye umri wa miaka 80 amekaa madarakani kwa miaka 43 na utawala wake ndio mrefu zaidi katika viongozi waliokaa muda mrefu madarakani walioko hai duniani ukiwaondowa watawala wa kifalme.

Picha: How Hwee Young/Getty Images

Alitwaa madaraka kutoka kwa Francisco Macias Nguema ambaye mwaka 1968 aliingia madarakani kama rais wa kwanza wa Guinea baada ya uhuru kutoka Uhispani na baadae kujitangaza binafsi kuwa rais wa maisha.

Macias ambaye ni mjomba wa rais Obiang, aliuliwa kwa kupigwa risasi miezi miwili baada ya mapinduzi. Wapinzani wa rais Obiang wanasema kwamba chini ya utawala wa mkono wa chuma wa rais huyo Guinea ya Ikweta imekuwa ndiyo Korea Kaskazini ya barani Afrika.

Ukandamizaji

Kila uchao utawala huo wa kikatili unalaaniwa na kukosolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu ambayo yameorodhesha visa vya watu kukamatwa ovyo ovyo, wapinzani kushikiliwa katika magereza yenye mazingira mabaya na magumu pamoja na kamatakamata inayofanywa kila mara dhidi ya watu wanaoshukiwa kuwa wanapanga njama dhidi ya serikali.

Katika Guinea ya Ikweta kuna chama kimoja tu cha upinzani kilichoruhusiwa na kwa maana hiyo rais Obiang anadhibiti kikamilifu mwelekeo wa siasa ya nchi hiyo.

Mnamo mwaka 2016 alichaguliwa tena kurudi madarakani kwa asilimia 93.7 ya kura. Katika uchaguzi wa bunge ambao pia unafanyika Jumapili chama chake cha Democratic Party of Equatorial Guinea -PDGE kinategemewa tena kurudi madarakani.

Makamu wa rais-Teodoro Nguema Obiang ManguePicha: Jerome Delay/AP Photo/picture alliance

Chama hicho kilikuwa kikishikilia viti 99 kati ya 100 vya bunge na katika baraza la Seneti kinadhibiti viti vyote 70.

Ama kwa upande mwingine mwanawe wa kiume Teodoro Nguema Obiang Mangue anayefahamika zaidi kama Teodorin kwa kiasi kikubwa anaangaliwa kama ndiye atakayemrithi babake akishikilia hivi sasa nafasi ya makamu wa rais.