1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Nkurunziza atamba kurejea Burundi

Admin.WagnerD15 Mei 2015

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza anasema amerejea nchini humo, huku naibu kiongozi wa mapinduzi akikiri kuwa jaribio la kumuangusha Nkurunziza limeshindwa. Umoja wa Mataifa umetaka kurejeshwa haraka utawala wa sheria.

Burundi Präsident Pierre Nkurunziza
Picha: Reuters/T. Mukoya

Mshauri mwandamizi wa mawasiliano wa rais Willy Nyamwitwe, alisema Nkurunziza amerejea nchini humo, lakini hakutoa maelezo zaidi kwa kile alichosema ni sababu za kiusalama. Nkurunziza alikuwa nchi jirani ya Tanzania kwa ajili ya mazungumzo ya kikanda siku ya Jumanatano wakati mapinduzi yalipotangazwa na Jenerali Godefroid Niyombere, na kufunika wiki kadhaa za maandamano dhidi ya jaribio la rais kutafuta muhula wa tatu.

Taarifa za kurejea kwa rais Nkurunziza hazikuweza kuthibitishwa na duru huru hata hivyo, na uwepo wake umeendelea kuwa kitendawili usiku wa Alhamisi. Lakini tangazo kwamba amerudi lilifuatia haraka na kukiri kwa naibu kiongozi wa mapinduzi Cyrille Ndayirukiye kwamba mapinduzi hayo yameshindwa. Ndayikuriye aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP, kuwa binafsi anatambua kuwa vuguvu lao limeshindwa.

Waandamanaji wanaompinga Nkurunziza wakishangalia baada ya kutangazwa kwa mapinduzi.Picha: Reuters/G. Tomasevic

Watiifu wadhibiti vituo muhimu

Mapema Alhamis, wanajeshi watiifu kwa rais walisema walizuwia mashambulizi mawili makubwa yaliyofanywa na wapinzani katika mapambano makali ya kudhibiti kituo chenye umuhimu wa kimkakati cha redio ya taifa. Miili ya wanajeshi watatu ilionekana ikiwa imelala mitaani karibu na eneo la mapigano hayo, ishara ya kwanza ya maafa katika kadhia hiyo ya mapinduzi. Kufikia mchana, mkurugenzi wa kituo hicho Jerome Nkokirantevye alisema wanajeshi watiifu ndiyo walikuwa wanakidhibiti kituo hicho.

Afisa mwanadamizi wa polisi alithibitisha taarifa hizo na kusema jana jioni kuwa wanajeshi wanaounga mkono mapinduzi walisambaratika baada ya mashambulizi yao dhidi ya Televisheni ya taifa RTNB na jengo la redio katika mji mkuu kukandamizwa. Alisema baadhi ya waasi tayari wamejisalimisha na wengine walikimbia.

Tangazo la mapinduzi la Jumatano lilisababisha ukosoaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia, na kuibua hofu ya kurejea katika vurugu kubwa katika taifa hilo maskini, ambalo bado linaedelea kuhisi athari za vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 13 vilivyomalizika mwaka 2006, na kugharimu maisha ya maelfu ya Warundi.

Kibonzo hicho kilichorwa na Said Michael kutoka Tanzania, kuelekea mkutano wa kilele wa kujadili mgogoro wa Burundi.Picha: Said Michael

Baraza la Usalama laonya

Marekani ilisisitiza Alhamis kuwa Nkurunziza ndiye rasi halali wa Burundi bado. Nalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana katika kikao cha dharura siku ya Alhamis, lililaani jaribio hilo la mapinduzi, na kutaka kurejeshwa haraka kwa utawala wa sheria na kufanyika kwa uchaguzi kwa kuzingatia makubaliano ya Arusha.

Katika taarifa iliyosomwa na Raimonda Murmokaite, balozi wa Lithuania katika Umoja wa Umoja wa Mataifa, na rais wa barala hilo kwa mwezi wa Mei, baraza hilo lenye wanachama 15 lilieza utayarifu wake kuchukulia hatua vitendo vya vurugu nchini Burundi vinavyotishia amani na usalama.

"Wanachama wa baraza la usalama wamelaani machafuko nchini Burundi na hasa wamewalaani wanaochochea vurugu za aina yoyote dhidi ya raia, na wale wanaotaka kutwaa madaraka kwa njia zisizohalali," alisema Murmokaite.

"Wanachama wa baraza la usalama wametoa wito kwa pande zote kutotumia vurugu na kutoa kipaumbele kwa amani na usalama. Baraza pia limerejelea uungaji wake mkono wa juhudi la mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Said Djinnit, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki."

Wakimbizi wa Burundi waliowasili nchini Tanzania kufuatia machafuko yanayoendelea nchini mwao.Picha: DW/P. Kwigize

Maelf wakimbilia nchi jirani

Katika taarifa iliyotangazwa kupitia redioni, rais Nkurunziza alisema analilaani kundi la waliokula njama, na kuwashukuru wanajeshi wanaorejesha utengamano, na kwamba anawasamehe wanajeshi wanaoamua kujisalimisha. Umoja wa Mataifa unasema zaidi Warundi 70,000 wamekimbilia nchi jirani, na kuivuruga kanda hiyo yenye historia ya mapigano ya kikabila.

Wapinzani wanasema jaribio la rais kugombea muhula wa tatu linakiuka katiba na makubaliano ya amani yaliyokomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hukumu ya mahakama ya katiba hata hivyo, ilisema rais anaweza kusimama tena, ikibainisha kuwa muhula wake wa kwanza, alipochaguliwa na bunge badala ya kura ya wananchi, haukuhesabiwa. Lakini wakosaoji wanasema mahakama hiyo ina upendeleo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,ape,ape

Mhariri: Sudi Mnette