1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za Uchaguzi zapamba Moto

18 Julai 2016

Rais Barack Obama awahimiza wamarekani waache matamshi makali na jazba, katika wakati huu ambapo matumizi ya nguvu yanaonyesha kugubika kampeni za uchaguzi wa rais.

Bendera ya Marekani yateremshwa nusu mlingoti baada ya mauwaji ya Baton RougePicha: Reuters/J. Penney

Rais Barack Obama anasema chanzo cha mauwaji ya maafisa watatu wa polisi huko Baton Rouge,Louisiane,bado hakijulikani. Ni kisa cha karibuni zaidi miongoni mwa visa vya mauwaji dhidi ya wasimamizi wa sheria,ikiwa ni pamoja na polisi kumpiga risasi bwana mmoja mweusi huko Baton Rouge na kuuliwa maafisa watano huko Dallas.

"Sisi kama taifa tunabidi kupaza sauti na kusema kinaga ubaga hakuna kinachohalalisha mashambulio dhidi ya wasimamizi wa sheria" amesema rais Obama katika taarifa aliyoitoa ikulu mjini Washington.

Rais Obama amesema hayo mnamo mkesha wa mkutano mkuu wa chama cha Republican ambapo Donald Trump atateuliwa rasmi kuwa mgombea wa chama hicho kwa uchaguzi wa rais.Tajiri huyo daima amekuwa akitumia matumizi ya nguvu yanayotokea Marekani kudai Marekani inahitaji uongozi mpya na mara nyingi hufika hadi ya kutumia maneno makali kushadidia hoja zake.

Obama ahimiza Moyo wa Mshikamano na sio wa Mtengano

Rais Obama amewatolea wito wanasiasa wanaoshiriki katika mikutano mikuu,maafisa waliochaguliwa na makundi mengine ya kisiasa yapime wanayoyasema na kupunguza jazba kwa lengo la kuimarisha umoja wa nchi na sio mtengano.„Tunabidi kupima maneno yetu na kufungua nyoyo zetu-sote. Tunahitaji kile tulichokishuhudia Dallas, pale jamii walipokusanyika kwa lengo la kurejesha na kuimarisha umoja na maelewano.Tunahitaji aina ya juhudi kama zile tulizoziona wiki hii katika mikutano kati ya viongozi wa jamii na polisi-nilihudhuria baadhi ya mikutano hiyo na kuwaona watu wa nia njema wakihimiza ushirikiano ili kupunguza matumizi ya nguvu katika jamii. Hicho ndicho tunachokihitaji kwasasa. Na ni jukumu letu kuhakikisha tunakuwa sehemu ya ufumbuzi na sio ya tatizo."

Rais Barack Obama akizungumzia wimbi la mauwaji nchini MarekaniPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Martin

Chanzo cha mauwaji ya Baton Rouge hakijulikani

Mapema jana rais Obama alizungumza na gavana wa jimbo la Louisiana John Bel Edwards na meya wa Baton Rouge Kip Holden ili kujua mepya kuhusu uchunguzi unaoendelea kuhusu mauwaji na kuahidi msaada wa serikali kuu. Kipindi kizima cha wiki iliyopita rais Obama alishughulika kupunguza mivutano na kurejesha hali ya kuaminiana kati ya polisi na jamii.

Polisi wapiga doria Baton RougePicha: Reuters/J. Penney

Julai saba iliyopita,mwanajeshi wa zamani alifyetua risasi mjini Dallas na kuwauwa maafisa watano na kuwajeruhi wengine saba. Mwanajeshi huyo mstaafu alikuwa mmarekani mweusi aliyesema amedhamiria kuwauwa hasa maafisa wa kizungu.

Mauwaji ya polisi mjini Dallas na Baton Rouge yamefuatia kisa cha kupigwa risasi wamarekani wawili weusi na polisi,Alton Sterling huko Baton Rouge na Philando Castile katika kitongoji cha St.Paul Minnesota-mauwaji yaliyopelekea maandamano kuitishwa katika kila pembe ya marekani. Polisi wa Dallas walikuwa wakiwalinda waandamanaji katika mji huo,walipofyetuliwa risasi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga