1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

030810 USA Irak Obama

Abdu Said Mtullya3 Agosti 2010

Rais Barack Obama aitekeleza ahadi ya kuyaondoa majeshi ya Marekani kutoka Iraq.

Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: AP

Rais Barack Obama amesisitiza kwamba askari wa Marekani wataanza kuondoka Irak kuanzia mwishoni mwa mwezi huu.

Rais Obama aliyasema hayo jana Atlanta Georgia. Rais Obama anaitekeleza ahadi aliyoitoa wakati alipokuwa anagombea urais wa Marekani.

Obama aliahidi kuvimaliza vita vya Irak kwa njia ya kuwajibika.Na mara tu baada ya kuingia madarakani rais Obama alitangaza mkakati mpya juu ya kuyakabidhi mamlaka kamili kwa watu wa Irak. Alieleza wazi kwamba jukumu la mapambano kwa wanajeshi wa Marekani litamalizika tarehe 31 mwezi agosti mwaka 2010.

Katika kuitekeleza ahadi ya rais Obama askari wa kwanza alfu 90 wataondoka Irak mwishoni mwa mwezi huu licha ya ongezeko la umwagikaji damu katika miji kadhaa ya Irak mnamo siku za hivi karibuni.

Katika hotuba aliyoitoa kwa mashujaa wa vita Atlanta, Georgia rais Obama alieleza kuwa Marekani itamaliza operesheni za kivita na hatua kwa hatua mpango wa misaada na mafunzo utatekelezwa.

Rais Obama pia amearifu kwamba Marekani imeshafunga mamia ya vituo vyake vya kijeshi na imevikabidhi baadhi kwa majeshi ya wazalendo wa Irak.

Rais Obama pia amesema kwamba Marekani inaondoa sehemu kubwa ya zana zake za kijeshi kutoka Irak.

Rais Obama anatumai kwamba hatua aliyoichukua itazingatiwa kuwa ni ushindi na wananchi wake.Hayo yanatokana na kutambua kwamba vita vya Irak haviungwi mkono na wamarekani wengi.

Tokea majeshi ya Marekani yaivamie Irak, askari 4400 wameuawa. Na wengine zaidi ya alfu 30 wamerudishwa nyumbani wakiwa majeruhi kimwili na kiakili.

Mnamo mwaka wa 2003 rais wa Marekani wa wakati huo George W.Bush alitoa amri ya kuivamia Irak kwa kutumia kisingizio kwamba dikteta wa nchi hiyo Saddam Hussein alikuwa na silaha za maangamizi.

Alipokuwa seneta,Obama alikuwa miongoni mwa maseneta wachache waliovipinga vita vya Iraq. Baada ya kuchaguliwa kuwa rais Obama aliahidi kuvimaliza vita vya Irak haraka.

Hatahivyo baadhi ya watu wana mashaka juu ya uamuzi wa rais Obama.Jenerali wa zamani wa Marekani Barry McCaffery amesema uamuzi wa kuyaondoa majeshi ya Marekani kutoka Irak ni sahihi lakini amesema kuwa nchi hiyo bado inakabiliwa na matatizo mengi. Amesema nchi hiyo mpaka sasa haina serikali.

Hatahivyo rais Obama amesema kiwango cha umwagikaji damu na mauaji kimepungua nchini Irak na anadhamiria kuitekeleza ahadi yake ya kuyaondoa majeshi yote kutoka Irak hadi mwishoni mwa mwaka ujao.Lakini wanajeshi alfu 50 wa Marekani wataendelea kuwapo nchini Irak hadi wakati huo.

Mwandishi/Silke Hasselmann/ÜMDR/

Tafsiri/Mtullya Abdu/

Mhariri/Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW