1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama amwonya Gaddafi

19 Machi 2011

Baada ya Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kuifunga anga ya Libya, Rais Barack Obama ameonya kuwa Marekani inaweza kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya kiongozi huyo wa Libya ikiwa hataacha kuwashambulia watu wake.

Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: AP

Rais Obama amesema yaliyotamkwa katika azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kuwalinda raia nchini Libya siyo masuala ya kujadiliwa. Amesema ikiwa Kanali Gaddafi hatalitekeleza azimio la Baraza la Usalama jumuiya ya kimataifa itamchukulia hatua na azimizo hilo litatekelezwa kwa njia ya nguvu za kijeshi.

Rais Obama amesema katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya televisheni, kwamba Gaddafi lazima aache mashambulio yote.Kiongozi huyo wa Marekani amemtaka Kanali Gaddafi ayaamrishe majeshi yake ili yaache kuelekea Benghazi na ayaondoe kutoka miji ya Ajdabiya, Misrata na Az Zawiya.

Maseneta wa chama cha Republican, MarekaniPicha: AP

Wabunge wataka mjadala rasmi

Hata hivyo, wabunge wa Marekani wamesema wanataka mjadala rasmi ufanyike na kura ipigwe juu ya kuidhinisha hatua zozote za kijeshi za kuchukuliwa dhidi ya Libya. Wabunge hao wameeleza kuwa katiba ya Marekani imelipa bunge mamlaka ya kutangaza vita na siyo Rais.

Seneta wa chama cha Republican, Richard Lugar amesema Rais hapaswi kuamua juu ya vita dhidi ya Libya bila ya wawakilishi wa wananchi kupiga kura. Lakini onyo lililotolewa na Rais Obama juu ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Libya limeungwa mkono mara moja na Ufaransa, Uingereza na nchi za Kiarabu.

Wananchi wa Libya wakiwa wamenyanyua juu benderaPicha: AP

Libya yatangaza kusimamisha mashambulizi

Wakati huo huo, nchini Libya utawala wa Gaddafi umesema kuwa umesimamisha mashambulio, lakini pana taarifa kwamba mashambulio bado yanaendelea katika baadhi ya maeneo fulani. Juu ya hayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton amesema jumuiya ya kimataifa haitavutiwa na kauli. Amesema kinachotakiwa ni hatua thabiti. Bibi Clinton amesema ameziona taarifa za vyombo vya habari zilizotolewa na serikali ya Libya juu ya kusimamisha mashambulio.

Lakini ameeleza kuwa hali inaendelea kubadilika kwa haraka. Hata hivyo, ametamka kuwa angelipendelea kuona hatua thabiti, lakini amesema hali bado haijawa wazi. Waziri Clinton amesema Marekani itashirikiana na washirika wake katika jumuiya ya kimataifa ili kumshinikiza Gaddafi aondoke na pia itaendelea kuyaunga mkono matakwa halali ya watu wa Libya.

Na Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Susan Rice amesema utawala wa Gaddafi unalikiuka azimio la Baraza la Usalama juu ya kusimamisha mashambulio. Balozi huyo alikuwa anajibu swali, iwapo utawala wa Gaddafi unakiuka azimio la Umoja wa Mataifa.

Mkutano kuhusu Libya kufanyika Ufaransa

Rais wa Ufaransa, Nicolas SarkozyPicha: picture alliance/abaca

Habari kutoka Paris zinasema Ufaransa inaitisha kikao muhimu leo kujadili hali ya Libya, kitakachohudhuriwa pia na wawakilishi kutoka Umoja wa nchi za Kiarabu, Umoja wa Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton. Na duru za kibalozi za Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa zimeashiria kwamba hatua za kijeshi dhidi ya Libya zinakaribia sana kuchukuliwa, yumkini baada ya kikao cha mjini Paris.

Mwandishi:Mtullya Abdu/AFPE/ZAR/ RTRE
Mhariri:Grace Patricia Kabogo