Iran yaendelea na mpango wa kurutubisha madini ya uranium nchini.
10 Februari 2010Mafundi stadi wa Iran wanatayarisha mitambo ili kuanza kurutubisha madini ya uranium hatua ambayo imemfanya rais Barack Obama wa Marekani atoe onyo juu ya kupitishwa vikwazo zaidi dhidi ya Iran.
Sambamba na mafundi stadi hao kuanza matayarisho ya shughuli za kurutubisha madini ya Uranium Iran imesema inaamini pana uwezekano wa kufikiwa makubaliano na nchi za magharibi juu ya mpango wa kubadilishana nishati ya nyuklia. Mkuu wa shirika la nyuklia la Iran bwana Ali Akbar Salehi amesema kwamba mapatano yanaweza kufikiwa .
Lakini matamshi yake yametafsiriwa kuwa na maana ya kusisitiza msimamo wa nchi yake wa hivi karibuni juu ya kurutubisha madini ya uranium nchini. Nchi za magharibi zinaitaka Iran iyapeleke madini hayo nje ili yarutubishwe.
Bwana Salehi amesema madini ya uranium yaliyorutubishwa yanaweza kusimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia IAEA.Uamuzi wa Iran kuanza matayarisho ya kurutubisha madini hayo umemfanya rais Obama wa Marekani aonye juu ya kupitishwa vikwazo thabiti dhidi ya Iran.
Rais Obama amesema mazungumzo yanayofanyika baina ya mataifa sita yanaendelea kwa haraka. Mazungumzo hayo yanafanywa na wajumbe wa Marekani,Urusi,China Ufaransa,Uingereza na Ujerumani.Rais Obama amesema katika wiki zinazofuata, mataifa hayo yatashughulikia hatua za vikwazo dhidi ya Iran kwa sababu nchi hiyo bado inaendelea kupinga takwa la jumuiya ya kimataifa juu ya Iran kuacha kabisa kurutubisha madini ya Uranium. Rais Obama amesema Iran imeamua kusonga mbele na mpango wa kurutubisha asilimia 20 ya madini ya Uranium hatahivyo ameeleza kuwa mlango wa mazungumzo bado upo wazi.
Rais Obama amesema jumuiya ya kimataifa itaangalia njia mbalimbali ili kuashiria kwa Iran kwamba njia inayochukuliwa na nchi hiyo haikubaliki.
Rais huyo amesema jumuiya ya kimataiafa inasonga mbele haraka kuelekea kwenye lengo la kuiwekea Iran vikwazo baada ya nchi hiyo kuthibitisha kwamba imeanza shughuli za kurutubisha asilimia 20 ya madini ya Uranium.
Rais Obama amesema msimamo wa Iran wa kuupinga mpango uliofikiwa kutokana na juhudi za Umoja wa Mataifa juu ya madini hayo kurutubishwa nje ni, ishara kwamba Iran inadhamiria kuunda silaha za nyuklia.
Lakini Iran imesema kwamba mpango wake wa nyuklia unalenga shabaha za amani tu. Iran imesisitiza kuwa mpango wake ni wa kuzalisha nishati ya nyuklia ili kukidhi mahitaji ya tiba kwa ajili ya wagonjwa zaidi ya alfu 850.
Mwandishi/Mtullya Abdu/ZA/RTRE
Mhariri/Abdul-Rahman