Rais Obama awasilisha mpango wa kufufua uchumi
9 Septemba 2011Katika hotuba yake hiyo iliyokuwa ikingojewa kwa hamu, Obama ameliambia bunge, lengo ni kufufua uchumi wa Marekani uliozorota, kutoa nafasi mpya za ajira na kuwapa vijana matumaini.
Kiini cha mpango huo ni kupunguza gharama za ruzuku ya serikali kwa wale wasiojiweza na kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu na miundo mbinu. Lengo pia ni kufanya mageuzi katika mfumo wa kodi, ili wenye pato kubwa kabisa wasiwe wenye kunufaika zaidi. Kinachohitajiwa amesema, ni mfumo utakaohakikisha kodi ya haki kwa kila mmoja. Obama vile vile, amependekeza kupunguza kodi ya pato kwa nusu. Hata kampuni zipunguziwe kodi ili ziweze kutoa nafasi mpya za ajira au kuongeza mishahara ya wafanyakazi wake.
Rais Obama ameliomba bunge kuuidhinisha mpango huo. Amesema, Marekani hivi sasa ikikabiliwa na mzozo wa kitaifa, Warepublikan na Wademokrat hawana budi kuwajibika.