1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama awataka wamarekani wachukue hatua za kuleta mageuzi katika mfumo wa afya.

Abdu Said Mtullya10 Septemba 2009

Rais Obama ataka mageuzi haraka lakini Republican wanahofia gharama.

Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: AP

Rais Barack Obama amewataka wamerakani wachukue hatua ili kuleta mageuzi katika mfumo wa bima afya nchini.

Rais Obama aliwaambia wabunge wa nchi yake kwamba kushindwa kuleta mageuzi hayo kulilitosa taifa katika hali ngumu.

Suala la kuleta mageuzi katika mfumo wa afya nchini Marekani limo katika moyo wa rais Obama kama ilivyodhihirika katika hotuba yake kwa wabunge wa nchi yake. hapo jana. Hotuba ya Obama iliwatoa watu ngozi ya kimbimbi. Rais huyo alisema kuwa yeye siyo rais wa kwanza wa Marekani kulizingtia suala la mageuzi ya mfumo wa afya.lakini amesema amejizatiti kuwa wa mwisho.

Hotuba ya rais Obama iliyochukua muda wa dakika 45 ulikuwa hasa ni mwito kwa wananchi na wabunge wake.

Watu karibu milioni 50 hawana bima ya afya nchini Marekani jambo ambalo kwa rais Obama ni dalili ya kushindwa kwa taifa zima. Amesema kila mwananchi wa Marekani anapaswa kuwa na bima ya afya,bila ya kujali kipato chake. Obama amewahakikishia wananchi wake kwamba haitakuwa lazima kwa mtu kubadili bima yake ya afya ikiwa ameridhika na aliyokuwa nayo.

Kwa mujibu wa mageuzi ambayo Obama anakusudia kuyaleta katika mfumo wa afya, wastaafu hawatakuwa na haja ya kuwa na wasiwasi kwa sababu ni serikali itakayolipia bima hiyo.

Lakini hotuba ya rais Obama haikushangiliwa sana na baadhi ya wajumbe wa chama cha Republican.Mjumbe mmoja Joe Wilson hata alidiriki kumwita rais Obama kuwa ni mwongo. Hatahivyo mjumbe huyo alimtaka radhi rais Obama kwa kauli yake ya kuropokwa.

Wajumbe wa chama cha Republican wamesema kuwa mradi wa rais Obama utakuwa wa gharama kubwa zaidi. Mjumbe mmoja wa chama hicho Charles Boustany ambae ni daktari wa upasuaji amesema sasa panahitajika mwanzo mpya wa utakaozishirikisha pande zote mbili.

Lakini mjumbe huyo alihoji kuwa, kwa mtu kuacha bima aliyokuwanayo sasa na kujiunga na bima ya afya itakayogharamiwa na serikali halitakuwa suluhisho. Amesema mfumo unaokusudiwa kuletwa na rais Obama utakuwa wa gharama kubwa sana.

Lakini mjumbe mwengine wa chama cha Republican seneta John McCain amesema kuwa inawezekana kukubaliana juu ya mambo mengi na kushirikiana. Seneta McCain ameeleza kuwa watu wa Republican pia wanataka mageuzi kwa sababu wanatambua kuwa mfumo uliopo ni mbovu.

Wajumbe wa chama cha Republican hawakushangilia sana hotuba ya Obama kwa sababu ya kuhofia gharama zitakazofikia dola bilioni 900 katika miaka 10 ijayo. Lakini rais Obama amesema wakati wa kubishana umeshapita.

Mwandishi: Mrakwald,Nicole/Washington (HR/Abdul Mtullya

Mhariri:M.Abdul-rahman