1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama kuhutubia kuhusu mageuzi ya bima ya afya

Kabogo Grace Patricia9 Septemba 2009

Hotuba hiyo ya mpango wake wa mageuzi ya huduma ya bima ya afya ataitoa kwenye bunge la Marekani yaani baraza la Congress.

Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: AP

Rais Barack Obama wa Marekani amesema atawapa Wamarekani ukweli unaotakiwa baada ya kufafanua mpango wake wa kurekebisha mfumo wa bima ya afya nchini humo, katika hotuba yake muhimu atakayoitoa usiku wa leo kwenye bunge la Marekani yaani baraza la Congress.

Akihojiwa hii leo na kituo cha televisheni cha ABC, Rais Obama alisema Wamarekani watapata ufafanuzi zaidi kuhusu fikra zake juu ya njia sahihi kuelekea mbele.

Kauli hiyo ya Rais Obama ambaye amekuwa akikabiliwa na shinikizo la kuelezea jinsi atakavyofanya mageuzi ya mfumo wa huduma za bima ya afya nchini humo, ameitoa kabla ya hotuba yake kwa Bunge la Marekani-Congress, ambayo inaonekana kuwa muhimu ili kuokoa mpango wake wa kufanyia marekebisho mfumo wa huduma za afya nchini humo, baada ya mpango huo kupigiwa kelele na wabunge wa chama cha Republican kwa wiki kadhaa. Hotuba hiyo ya Rais Obama, inategemewa kuwa na urefu wa dakika 35. Zaidi Rais Obama anasema:

''Hivyo dhamiria ya hotuba hii ni A): kuhakikisha kuwa watu wa Marekani wanaelewa vizuri kuhusu kitu tunachopendekeza. B): Kuhakikisha kuwa wanachama wa Democrat na Republican wanaelewa kuwa niko wazi kwa mawazo mapya, siyo kwamba hatutaki kubadilika na tuna itikadi kuhusu hili, lakini tunakusudia kupata kitu kitakachofanyika mwaka huu.''

Endapo atafanikiwa kupitisha muswada huo wa mageuzi ya bima ya afya na kuwanufaisha Wamarekani milioni 46 wasio na bima ya afya, Rais Obama ataweza kuhisi amejipatia mafanikio makubwa ambayo yaliwakwamisha marais wengi waliotetea mageuzi katika vizazi vingi vilivyopita. Ikulu ya Marekani-White House, imekuwa ikisema kwamba kazi ya kuwanufaisha Wamarekani wote kwa kuwapatia huduma ya bima ya afya imekuwa ikiendelea kwa vizazi kadhaa na haijawahi kufanikiwa.

Huku wabunge wa Republican wakiuwekea kishindo kikubwa mpango huo kama ushahidi serikali inajaribu kuchukua mfumo huo na kuanzisha mfumo wa huduma za afya za Ulaya, uwezekano wa kupitisha unakuwa wa wasiwasi. Rais Obama anatarajiwa kutetea hatua ya serikali kushindana na wadau binafsi wa bima kuwasaidia Wamarekani ambao hawana bima ya afya. Rais huyo wa Marekani pia anatumai kuondoa fikra zilizopo kuwa serikali itachukua suala la huduma ya afya, zinazozungumzwa na baadhi ya wakosoaji wake.

Rais Obama amesema miongoni mwa fikra zinazokebehi ambazo hotuba yake itaziondoa ni uzushi wa kuwaadhibu kifo watu wazee au wagonjwa sana kutokana na huduma itakayotolewa, pamoja na mazungumzo ya mageuzi ambayo yatatoa huduma ya bima ya afya kwa wahamiaji wanaoishi nchini humo isivyo halali.

Mwandishi: Grace Patricia kabogo (AFP)

Mhariri:Abdul-Rahman