1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi 10 wauawa nchini Afghanistan.

23 Juni 2010

Jenerali McChrystal aomba radhi kuhusu matamshi yake, adaiwa kuandika barua ya kujiuzulu.

Jenerali Stanley McCrystal atakutana ana kwa ana na rais Obama kuhusu matamshi yake.Picha: picture-alliance/dpa

Kamanda mkuu wa Marekani anayeongoza kikosi cha wanajeshi nchini Afghanistan, Jenerali Stanley McChrystal anatarajia kujua hatima yake leo baada ya kuitwa na rais Barack Obama kufafanua matamshi yake ya kuwakosoa viongozi wakuu serikalini. McChrystal na rais Obama wamesema kwamba maandishi yaliyochapishwa katika jarida la Rolling Stone yalionyesha uamuzi mbaya.

Jenerali Stanley McChrystal anatarajiwa kukutana ana kwa ana na rais Barack Obama na atakutana pia na wale aliowakosoa katika mkutano wa kila mwezi katika ikulu ya Marekani kuhusiana na masuala ya Afghanistan na Pakistan. Bw. McChrystal anatarajiwa kuwasili mjini Washington mwendo wa asubuhi wakati mkutano huo kuhusu Afghanistan na Pakistan unapotarajiwa kuanza lakini haijabainika wazi ikiwa mazungumzo ya ana kwa ana yatafanyika kabla au baada ya mkutano huo.

Kuvunjika moyo Jenerali McChrystal kulidhihirika wakati wa mkutano wake wa kwanza na rais Obama. Jenerali huyo alihisi kwamba rais Obama hakuwa na haja. Leo anaweza pia kukutana na waziri wa ulinzi Robert Gates. Jenerali huyo wa Marekani aliomba radhi kutokana na makala iliyoandikwa katika jarida la Rolling Stone yenye mada, ‘Jenerali aliyeasi’ iliyoandikwa na Michael Hastings na itakayochapishwa siku ya Ijumaa wiki hii. Aliomba radhi na kusema matamshi yake yalionyesha ukosefu wa uadilifu na kwamba yalikuwa makosa yaliyoashiria uamuzi mbaya na kamwe hayakufaa kutokea.

Vyombo vya habari nchini Marekani vinasema kwamba tayari Jenerali McChrystal ametuma barua ya kujizulu lakini itategemea uamuzi wa rais Obama ikiwa ataikubali na hakujatolewa matamshi yoyote rasmi kuhusiana na taarifa hiyo.

Rais wa Marekani, Barack Obama atakutana na Jenerali McChrystal kabla ya kutoa uamuzi wake.Picha: AP

Msemaji wa ikulu ya Marekani, Robert Gibbs amesema rais Obama alikuwa amekasirika na kwamba jenerali McChrystal amefanya makosa makubwa na kwamba uchaguzi wa hatua dhidi yake upo mezani na anashangaa jenerali huyo alikuwa akifikiria nini.

Wabunge kadhaa wa Marekani wanamtaka jenerali McChrystal aondolewe huku rais Obama akilazimika kuchagua kati ya kuendeleza uongozi nchini Afghanistan wakati huu na uongozi wa umoja utakaomuonyesha kama amiri jeshi mkuu anayeheshimika.

Msemaji wa kundi la Taliban amesema kuitwa kwa Jenerali Stanley McChrystal ni ishara nyingine ya mwanzo wa kushindwa kisiasa kwa sera ya Marekani nchini Afghanistan lakini msemaji wa rais Hamid Karzai wa Afghanistan, Waheed Omer amesema anamuunga mkono jenerali McChrystal.

Wakati huo huo huko nchini Afghanistan, wanajeshi kumi wa NATO wameuawa katika mashambulio ya wapiganaji na kwenye ajali ya helikopta iliyoanguka huko Kandhahar, huku kukiwa na dalili za mpasuko katika jumuiya hiyo ya NATO. Vifo hivyo vinaiweka idadi ya waliouawa kufikia 65 mwezi huu na 285 mwaka huu kulingana na takwimu ya shirika la habari la AFP.

Mwandishi, Peter Moss /AFP

Mhariri, Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW