Rais Obama na mkakati mpya kuhusu hali nchini Afghanistan
30 Septemba 2009Ishara ya umuhimu wa mkutano, huo na usiri wake inajitokeza wazi, ukiangalia orodha ya waliopata mualiko na eneo mkutano huo unafanyika. Eneo ni chumba chenye usalama mkuu katika Ikulu ya Marekani.
Mkutano huo unaolenga kutathmini mkakati wa Marekani nchini Afghanistan, na wapi panapohitajika mabadiliko, hasa kuhusiana na swala la kuongezwa kwa idadi ya wanajeshi, maamuzi yake yatachangia iwapo Marekani itakuwepo Afghanistan kwa muda mrefu.
Rais Obama atakaa mezani na washauri wake wakuu, ikiwemo, Makamu wa rais Joe Biden, Waziri wa mambo ya nchi za nje Hillary Clinton, na Robert Gates anayesimamia wizara ya ulinzi. Generali Stanley McChrystal, kamanda mkuu wa majeshi ya Marekani Afghanistan, pia anasemekana atahudhuria au kama sivyo atashiriki katika majadiliano hayo kwa njia ye video.
Rais Obama amekuwa na shinikizo nyingi, kubadili mweleko nchini Afghanistan, na hasa baada ya ripoti ya McChrystal kufichuka. McChrystal alikuwa anaonya katika muda wa mwaka mmoja ujao, Marekani huenda ikashindwa huko Afghanistan iwapo haitaongeza idadi ya wanajeshi. McChrystal anasemekana ameitisha wanajeshi wengine kiasi cha elfu 40 kukabiliana na uasi wa Taliban unaozidi.
Mkakati Afghanistan pia ulikuwa ndio ajenda katika mkutano wa Rais Obama na katibu mkuu wa Nato, Anders Rasmussen katika ikulu ya Marekani- alipoashiria kuwa Marekani inahitaji ushirikiano zaidi kutoka nchi za Ulaya.
Washirika wakuu wa Marekani Ulaya bado wana shaka, hasa kuhusiana na kuongeza idadi ya wanajeshi, Afghanistan. Jana Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung, alisema washirika wa NATO barani Ulaya wanafaa, kusubiri hadi pale Marekani itakapotoa mpango rasmi wa kuongezwa kwa wanajeshi Afghanistan.
Anders Rasmussen lakini alimhakikishia rais Obama kuwa majeshi ya NATO Afghanistan yataendelea kuwepo , hadi watakapokamilisha kazi iliyowapeleka nchini humo.
Kura ya maoni nchini Marekani zinaashiria kuwa Wamarekani wengi wamepoteza imani na vita hivyo Afghanistan. Ni changamoto hizi ndizo Rais Obama ataendelea kupima kabla ya kufanya maamuzi, wa mkakati ufaao nchini Afghanistan.
Mwandishi: Munira Muhammad/AFPE
Mhariri: Abdul-Rahman