1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Rais Rajapaksa wa Sri Lanka huenda akakimbia nchi

Sylvia Mwehozi
11 Julai 2022

Taarifa kutoka nchini Sri Lanka zinasema kuwa rais wa taifa hilo anayekabiliwa na mzozo amesafirishwa hadi kituo cha jeshi la wanaanga na kuibua uvumi kwamba huenda akakimbilia uhamishoni.

 Sri Lanka Feierlichkeiten zum Unabhängigkeitstag
Picha: picture-alliance/NurPhoto/T. Basnayaka

Rais Gotabaya Rajapaksa alikimbia Ikulu mjini Colombo chini ya ulinzi mkali wa wanajeshi wa majini siku ya Jumamosi, muda mchache baada ya maelfu ya waandamanaji kuvamia majengo ya Ikulu. Afisa mmoja mwandamizi wa kijeshi ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Rais huyo mwenye umri wa miaka 73 amechukua hifadhi katika kituo kimoja cha kijeshi kabla ya kupelekwa kwenye kambi ya anga ya Katunayake inayopakana na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bandaranaike.

Hapajakuwa na tarifa rasmi kutoka ofisi ya rais juu ya wapi alipo kiongozi huyo, lakini ripoti za vyombo vya habari vya Sri Lanka zinaashiria kwamba Rajapaksa huenda akakimbilia Dubai baadae leo.

Sri Lanka bado yakabiliwa na mkwamo wa kisiasaSpika wa bunge Mahinda Yapa Abeywardena amesema bunge litakutana tena Julai 15 na rais mpya atachaguliwa Julai 20 wakati rais Rajapaksa akijiandaa kuachia mikoba siku ya Jumatano. Spika Mahinda ameongeza kuwa "katika kikao cha viongozi wa chama kilichofanyika leo, ilikubaliwa kwamba hatua hii ni muhimu ili kuhakikisha serikali mpya ya vyama vyote inapatikana kwa mujibu wa Katiba na kuendeleza huduma muhimu."

Umati wa waandamanaji katika jengo la IkuluPicha: Eranga Jayawardena/AP Photo/picture alliance

Kwa upande wake, kiongozi wa upinzani Bw Sajith Premadasa ambaye chama chake cha  Samagi Jana Balawegaya SJB kinashikilia viti 54 katika bunge lenye jumla ya viti 225 amesema kuwa wako tayari kuunda serikali. Amesema kama upinzani wako tayari kutoa uongozi ili kutuliza nchi na kujenga uchumi. "Tutachagua rais mpya, waziri mkuu mpya na kuunda serikali". Chama hicho cha SBJ kimekuwa katika mazungumzo na makundi ya vyama vidogo ili kupata uungwaji mkono wa kiongozi wao Premadasa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Wang Wenbin amesema Beijing inafuatilia kwa ukaribu yanayoendelea katika taifa jirani.

"China inafuatilia kwa karibu maendeleo ya hivi karibuni ya hali ya Sri Lanka. Kama jirani na mshirika wa karibu, tunatumai kwa dhati kwamba sekta zote za Sri Lanka zitachukua maamuzi kwa maslahi ya kimsingi ya nchi na watu, kufanya kazi kwa pamoja na mshikamano kuondoka na matatizo na kujitahidi kurejesha utulivu wa kijamii, kufufua uchumi na kuboresha maisha ya watu mapema."

Kando na juhudi za kuunda serikali, msururu mrefu umeshuhudiwa hii leo wa watu kutembelea Ikulu kuliko baadhi ya foleni ndefu za Petroli katika maeneo ya mjini. Waandamanaji wanasema kwamba hawataondoka Ikulu hadi pale Rajapaksa atakapoachia rasmi madaraka.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW