1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Rousseff kujitetea kwa mara ya mwisho leo

4 Aprili 2016

Wakili mkuu wa Rais wa Brazil Dilma Rousseff atawasilisha leo (04.04.2016) hoja za mwisho mbele ya kamati inayochunguza uwezekano wa kiongozi huyo kushitakiwa.

Brasilien Präsidentin Dilma Rousseff
Rais wa Brazil, Dilma RousseffPicha: picture-alliance/dpa/F. Bizerra

Mwanasheria Mkuu Jose Eduardo Cardozo anatarajiwa kuwasilisha hoja mbele ya kamati hiyo yenye wanachama kutoka vyama mbalimbali vya siasa kwa mara ya mwisho kabla kupiga kura kuhusu ikiwa ipendekeze rais Rousseff ashitakiwe kwa madai ya kubadilisha mahesabu katika akaunti ya serikali kuficha matatizo ya kiuchumi yanayoikabili Brazil. Kikao hicho kinatarajiwa kuanza mwendo wa saa moja na nusu usiku.

Mapendekezo ya kamati hiyo yaliyopangwa kutangazwa Aprili 11 hayana mafumgano lakini yatatoa muelekeo wa jinsi kura itakavyopigwa katika baraza la wawakilishi kuhusu mustakabali wa Rousseff. Theluthi mbili ya kura za wajumbe wa baraza hilo, yaani kura 342, zinahitajika kuipeleka kesi ya rais huyo katika baraza la seneti. Kwa mujibu wa gazeti la Folha toleo la Jumapili, baraza la wawakilishi linatarajiwa kupiga kura Aprili 17.

Ratiba hiyo inampa rais Rousseff siku chache tu kutafuta uuungwaji mkono na kuokoa wadhifa wake. Kufuatia makubaliano yaliyofanyika kwa njia ya siri, anatarajiwa hivi karibuni kutangaza nafasi za uwaziri na nafasi za ajira serikalini zitakazotolewa kama zawadi kwa kuungwa mkono na bunge.

Hatima ya Lula kujulikana

Rousseff pia wiki hii atajua ikiwa mahakama ya juu kabisa ya Brazil itakubali rais wa zamani wa taifa hilo anayekabiliwa na kashfa, Luiz Inacio Lula da Silva, atajiunga na baraza lake la mawaziri.

Rais wa zamani wa Brazil, Inacio Lula da SilvaPicha: Reuters/P. Whitaker

Lula ni muhimu katika kuviunganisha vyama vya mrengo wa kushoto na kuvishawishi kuunda muungano unaopinga rais Rousseff kufunguliwa mashitaka, lakini amezuiwa kwa sababu anashutumiwa katika kesi inayohusiana na kashfa kubwa ya ubadhirifu wa fedha na hongo katika kampuni ya mafuta ya serikali, Petrobras.

Gabriel Petrus, mchambuzi katika shirika linalojihusisha na masuala ya siasa la Barral M Jorge Associates, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wiki hii pande zote mbili zitacheza karata zao kwa bidii na kuchukua hatua kwa umakini. "Wiki ijayo tutapa matokeo ya mapambano haya," akaongeza kusema mchambuzi huyo.

Rousseff anatuhumiwa kwa kuchakachua mahesabu ya akauti za serikali, madai ambao wachambuzi wengi wanayaona kuwa madogo na hayatoshi kuweza kumfungulia mashitaka. Hata hivyo rais huyo pia yuko katika kiti moto kwa mdororo wa kiuchumi na kashfa ya rushwa ya kampuni ya mafuta ya Petrobas. Huku umaarufu wa serikali yake ukiwa asilimia 10 na bunge likiwa halina uwezo wa kupitisha sheria, Rousseff tayari anaonekana hana nguvu.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe

Mhariri:Yusuf Saumu