Rais Sall wa Senegal akabiliwa na mbinyo kuhusu uchaguzi
15 Februari 2024Rais wa Senegal Macky Sall amekutana na baraza lake la mawaziri jana, wakati akizidi kukabiliwa na shinikizo la ndani na la kimataifa la kurejea katika kalenda ya uchaguzi uliocheleweshwa na kutatua mzozo mkubwa wa kisiasa.
Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano wa rais na baraza lake la mawaziri, ilizungumzia kidogo juu ya mzozo wa kisiasa unaoendelea. Ofisi ya rais, imechapisha video kwenye mitandao ya kijamii ikihimiza mazungumzo ya wazi ya kitaifa kabla ya uchaguzi.
Soma pia: Uchumi wa Senegal kuzorota kutokana na mkwamo wa kisiasa
Marekani, Ufaransa na Umoja wa Mataifa zimeunga mkono matakwa ya Wasenegali ya kutaka upigaji kura ufanyike haraka iwezekanavyo katika uchaguzi uliokuwa ufanyike Februari 25.
Kumekuwa na hofu kwamba mvutano huo unaweza kuenea na kusababisha ghasia zaidi. Watu watatu wameuawa katika maandamano, tangu Rais Sall alipotangaza kuchelewesha uchaguzi hadi Februari 25 Desemba.