1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia afanya mabadiliko katika baraza la mawaziri

9 Januari 2022

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri siku ya Jumamosi mnamo wakati akipambana kumaliza mivutano iliyopo ndani ya chama tawala CCM.

Tansania Präsidentin  Samia Suluhu Hassan
Picha: Eric Boniphase/DW

Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa na katibu mkuu Hussein Katanga, baadhi ya waliokuwa mawaziri wameachwa nje lakini pia baadhi ya wizara mpya zimebuniwa.

Nape Nnauye ambaye alifutwa kazi na mtangulizi wa rais Samia marehemu John Magufuli mwaka 2017, amerejeshwa tena kuwa waziri katika wizara ya Habari.

Masauni Yusuph Masauni ambaye awali alikuwa naibu waziri, sasa ameteuliwa kuwa waziri wa mambo ya ndani huku wizara ya Katiba na Sheria ikikabidhiwa waziri Simbachawene.

Palamagamba Kabudi na William Lukuvi waachwe nje

Waziri mwengine aliyeachwa nje ni William Lukuvi aliyekuwa akiongoza wizara ya Ardhi. Lukuvi ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe ambaye amekuwa mbunge na kudumu serikalini kwa miaka mingi.

Profesa Palamagamba Kabudi aliyesimamia wizara ya Katiba na Sheria ameachwa nje kwenye mabadiliko yaliyotangazwa.Picha: Getty Images/AFP/T.Karumba

Aliyekuwa waziri wa Afya Dorothy Gwajima, sasa atakuwa waziri katika wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wanawake na makundi Maalum.

Mageuzi ambayo Rais Samia amefanya yamejiri siku chache tu baada ya aliyekuwa spika wa bunge Job Ndugai kujiuzulu wadhifa wake kufuatia kutofautiana kauli hadharani.

Ndugai alijiuzulubaada ya kukosoa mikopo inayofanywa na serikali.

Katika jibu kwa Ndugai, Rais Samia alisema hakutarajia mtu anayeuongoza mhimili muhimu wa nchi kutoa kauli kama hiyo huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kukopa fedha kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

Aliyekuwa spika wa bune la Tanzania Job Ndugai alijiuzulu wadhifa huo wake baada ya kukosoa mikopo inayofanywa na serikali.Picha: DW/E. Boniphace

Kulingana na takwimu zilizochapishwa na benki kuu la Tanzania, katika mwezi wa Novemba mwaka uliopita, nchi hiyo ilikuwa ikidaiwa jumla ya dola bilioni 36.

Je, ipo mivutano ya ndani katika chama tawala CCM?

Mwezi uliopita, rais Samia aliwashutumu washindani wake ndani ya serikali kwa kujaribu kuupaka matope uongozi wake. Hatua hiyo ya nadra ilidhihirisha kuwepo mgawanyiko wa ndani katika chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Samia ambaye aliinuka na kuwa mwanamke wa kwanza rais nchini Tanzania mwezi Machi 2021, kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Pombe Magufuli, alidokeza mapema wiki hii kwamba angefanya mageuzi katika baraza lake la mawaziri, pale aliposema alitaka kuwaengua watu anaowashuku kushirikiana na washindani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Samia ambaye hata hivyo amejaribu kuachana na baadhi ya sera za Magufuli, lakini pia ametajwa kuwa ni ‘dikteta' na baadhi ya viongozi wa upinzani nchini mwake ambao bado wanatilia mashaka uhuru wa kisiasa na wa vyombo vya Habari nchini humo.

(RTR)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW