Rais Samia akosoa maandamano ya vurugu wakati wa uchaguzi
3 Novemba 2025
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amekosoa maandamano yaliyofanyika wakati wa uchaguzi, wa rais,bunge na madiwani, uliompa ushindi wa asilimia 98 ya kura, huku upinzani ukidai mamia ya watu wameuawa na vikosi vya usalama wakati wa maandamano hayo yaliyokumbwa na vurugu.
Ameyasema hayo huku chama kikuu cha upinzani CHADEMA kikiitaka Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC pamoja na Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi wa vurugu za baada ya uchaguzi zilizoshuhudiwa nchini humo.
Afisa wa chama hicho anayeshughulikia masuala ya kigeni Deogratias Munishi, amesema Samia na serikali yake inabeba damu za watanzania walioangamia wakati wa vurugu hizo.
"Watanzania sio wajinga, wamekuwa wakirekodi matukio yote na ndio maana hadi kufikia sasa Samia Suluhu Hassan na serikali yake wananuka damu ya watanzania. Hakuna taasisi yoyote inayoweza kuingilia kati, sio Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki wala SADC. Ni Umoja wa Mataifa na ICC pekee ndio wanaoweza kuujua ukweli ulipo na ndio maana tunatoa wito kwa kufanya uchunguzi wa haraka, wasichelewe kabla hali haijawa mbaya kufika mahali pa wao kujuta," alisema Rais Samia.
Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania INEC ilisema asilimia 87 ya watu walijitokeza kupiga kura licha ya ripoti ya waandishi habari wa shirika la habari la AFP pamoja na waangalizi wa kura wakisema sehemu kubwa ya vituo vya kupigia kura havikuwa na watu.