1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia akutana na Tundu Lissu Ubelgiji

17 Februari 2022

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alikutana na makamu mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema, Tundu Lissu, mjini Brussels, Ubelgiji siku ya Jumatano.

Belgien, Brüssel | Samia Suluhu Hassan, Präsidentin von Tansania in Brüssel
Picha: Sudi Mnette/Mohammed Khelef/DW

Kulingana na ofisi ya Rais Samia. Hii ni hatua moja inayoashiria kwamba huenda Lissu anajiandaa kurudi nyumbani kutoka uhamishoni.

Taarifa kutoka ofisi ya Rais Samia ilisema rais huyo aliamua kukutana na Lissu baada ya kwa ombi la kiongozi huyo. Taarifa hiyo iliendelea kusema kwamba "rais na Lissu walijadili masuala kadhaa yanayolihusu taifa la Tanzania." Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusiana na mazungumzo ya viongozi hao wawili.

Lissu ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais wa zamani wa Tanzania John Pombe Magufuli na serikali yake, alikwenda uhamishoni mwaka 2017 baada ya kupigwa risasi na kujeruhiwa na watu wasiojulikana katika mji mkuu wa nchi Dodoma.

Alirudi Tanzania Julai mwaka 2020 kushiriki uchaguzi mkuu ambapo alipoteza kwa Magufuli ila aliyapinga matokeo akidai kulikuwa na uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi huo. Alirudi tena uhamishoni Novemba 2020 baada ya kulalamika kuhusu kupokea vitisho vya kuuwawa.

Lakini Hassan ambaye alichukua madaraka baada ya kuaga dunia kwa Magufuli mwezi Machi mwaka 2021, amechukua hatua za kuboresha masuala ya haki za binadamu nchini Tanzania, ikiwemo kuondoa marufuku kwa vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa katika utawaka wa mtangulizi wake.

Baada ya Rais Samia kukutana na Lissu, nchini Tanzania kumekuwa na mjadala mkubwa unaoendelea huku wengi wakihisi kwamba hatua hiyo pengine ikawa mwanzo mpya wa kuanzishwa duru ya maridhiano na kutafuta majibu ya kudumu kuhusu masuala mbalimbali yanayopigiwa kelele na wapinzani.

Inavyojadiliwa na wengi Rais Samia ameanzisha hatua moja mbele na kugusa hisia za waliowengi waliosubiri kuona utawala wake unajipambanua kwa kukaribisha maridhiano ya kitaifa na kitendo chake tu cha kukutana na mwanasiasa, Lissu.

Kiongozi wa Chadema Tundu Lissu akiamkuana na Rais Samia HassanPicha: Sudi Mnette/Mohammed Khelef/DW

Tundu Lissu mwenyewe anaiyeishi ughaibuni kwa miaka kadhaa tangu anusurike katika jaribio la mauwaji, ameonesha jinsi alivyoridhishwa kwa namna Rais Samia alivyoonyesha utayari kuyashughulikia madai yao.

Mambo ambayo Lissu aliwasilisha kwa Rais Samia, ni pamoja kufutwa kwa kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kuondolewa marufuku kwa vyama vya upinzani kufanya siasa za wazi, kurejeshwa mchakato wa katiba mpya pamoja na kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi na kuhakikishiwa usalama wake pindi ataporejea nchini.

Chadema yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam ingawa haijatoa taarifa yoyote kuhusu mazungumzo hayo, katibu wake mkuu John Manyika ameandika katika mtandao wake wa Twitter akiuliza swali kwamba enzi mpya? Katiba mpya?

Hata hivyo, baadhi ya vyama vingine vya upinzani ingawa vimeikaribisha hatua hiyo, lakini vinasisitiza kuwa, kile kilichofanywa na Lissu ni kama hatua ya kuunga mkono majadiliano yaliyoanzishwa hivi karibuni kati ya vyama vya siasa, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa pamoja na ofisi ya Rais.

Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa pengine chadema imejitafakari na kuchanga vyema karata yake kwa kukutana na Rais kipekee. John Kitoka mchambuzi wa masuala ya kisiasa, anaamini kwamba dirisha la maridhiano sasa limefunguka.

Hayo yanajiri wakati ambapo hatma ya mwenyekiti Mbowe na washtakiwa wenzake ikitarajiwa kujulikana siku ya Ijumaa wakati Mahakama Kuu ya Tanzania itapokuwa ikitoa uamuzi wake. Uamuzi huo unapande mbili, mosi mahakama kutamka kama mwenyekiti huyo ana kesi ya kujibu au kuifutilia mbali.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW