Rais Samia alifanyia mageuzi madogo baraza lake la mawaziri
15 Agosti 2024Mabadiliko hayo ya baraza la mawaziri yamefanyika Jumatano, na kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Moses Kusiluka, mabadiliko makubwa yamefanyika katika wizara tatu, ambazo ni za Sheria na Katiba, Afya na ile ya Sera, Uratibu na Bunge.
Katika mabadiliko hayo, William Lukuvi, ameteuliwa kuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Sera, Uratibu na Bunge, wakati Profesa Kabudi, akiteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Katiba.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Wiraza ya Afya, sasa itasimamiwa na Jenista Mhagama, aliyekuwa Uratibu na Bunge.
Mabadilio mengine ni katika wizara ya Maliasili na Utalii, ambapo Pindi Chana anakwenda kushika nafasi ya Angellah Kairuki, ambaye kwa mujibu wa taarifa hiyo, ameteuliwa kuwa mshauri wa rais.
Mabadiliko haya, yameleta mawazo tofauti ambapo baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema, yanasababisha mtanziko wakati wengine wakisema, ni mkakati.
Je, ni mkakati wa kabla ya uchaguzi mkuu ?
Kama itakumbukwa, Januari mwaka 2022, Rais Samia, alifanya mabadiliko mengine kama haya katika baraza la mawaziri ikiwa ni miezi kadhaa tangu aingie madarakani, na aliwaondoa wateule wa hayati John Magufuli, Profesa Kabudi na Lukuvi katika baraza la mawaziri akieleza atawapangia kazi nyingine.
Lakini baada ya jana kuwarudisha, mabadiliko haya yaametafsiriwa kama yaliyoleta mtanziko, wakieleza kuwa rais haelezi kwa nini amemtoa waziri huyu na kumuweka sehemu nyingine, na kwa nini amewarudisha hali ambayo inaleta maswali na sintofahamu.
Pamoja na kubadili baraza la mawaziri kadhalika, Rais Samia amefanya mabadiliko mengine katika sekta za Sheria na Katiba, ambapo amemteua Hamza Johari, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akishika nafasi ya Eliezer Feleshi, Samwel Maneno ameteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu, huku Dk Ally posi akiteuliwa kuwa Wakili Mkuu wa Serikali.