1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia amehutubia bunge na kutoa dira ya serikali yake

John Juma Ripoti zaidi na Deo Makomba
22 Aprili 2021

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amelihutubia bunge la taifa hilo kwa mara ya kwanza tangu alipoapishwa kuwa rais hapo tarehe 19 Machi 2021.

Tansania | Amtseinführung Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: AP Photo/picture alliance

Kwenye hotuba yake bungeni mjini Dodoma, Rais Samia ameeleza kuhusu mwelekeo wa serikali ya awamu ya sita ambao ni kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya.

Ikiwa ni hotuba yake ya kwanza bungeni tangu alipoapishwa kuwa rais kufuatia kifo cha aliyekuwa mtangulizi wake John Pombe Magufuli, Samia amesema jitihada zaidi zinahitajika katika kukuza uchumi na vilevile kupambana na umasikini, akifafanua kwamba licha ya mafanikio yalioyoatikana, kasi ya ukuaji ingali ndogo.

Amebainisha kwamba sawa na nchi nyingine ambazo zimeathirika kutokana na janga la COVID-19, Tanzania vilevile imeathirika na uchumi wake umeshuka kutoka asilimia 6.9 hadi 4.7.

Mfahamu Rais Samia Suluhu Hassan

Kulingana na Samia, miongoni mwa vipaumbele vya serikali ni kuendelea kuboresha sera za uchumi na fedha.

Ndege ya shirika la ndege TanzaniaPicha: flickr/stevesaviation

Amesisitiza kuhusu kila mmoja kuwa na uhakika wa kupata matibabu kwa kuimarisha mifuko ya bima za afya.

Kuhusu shirika la ndege la Tanzania (ATCL) Rais Samia Suluhu amesema serikali yake inaangalia namna ya kulilea shirika hilo kimkakati ili liweze kujiendesha kwa ufanisi. Lengo la serikali kuhusu shirika hilo ni pamoja na kulitua mzigo wa madeni makubwa.

Vilevile amewaonya wale aliowataja kuwa ‘wachonganishi wa mtandaoni'. Akirejelea kifo cha mtangulizi wake hayati John Magufuli, Samia amesema taarifa rasmi waliyopewa kuhusu kifo cha kiongozi huyo ni matatizo ya moyo ambayo aliishi nayo kwa zaidi ya miaka kumi.

“Kuna watu mitandaoni wanasema fulani na fulani wamempa sumu. Kama wana taarifa waje tuwasikilize na taarifa zao,” amesema Rais Samia.

Kuhusu masuala ya uboreshaji wa demokrasia na uhuru nchini mwake, Rais Samia amesema ana mpango wa kukutana na viongozi wa kisiasa ili waweke mikakati ya kuendesha shughuli za kisiasa.

Rais Samia Hassan awaonya 'wachochezi' wa mitandaoni

This browser does not support the audio element.

Samia: Mimi na Magufuli tulikuwa kitu kimoja

Rais Samia amesema kuwa yeye na hayati Magufuli walikuwa kitu kimoja na kwa msingi huo mambo anayoyatekeleza yeye hivi sasa ni yale yaliyoachwa na mtangulizi wake ikiwa ni pamoja na kulinda tunu za Taifa. 

Hata hivyo Rais Samia amesema Tanzania imekuwa ikilalamikiwa na wawekezaji kuwa na urasimu na hivyo kuwafanya wawekezaji kushindwa kuwekeza Tanzania na kwamba katika awamu yake atahakikisha kuna kuwa na mazingira mazuri yatakayowavutia wawekezaji. 

Aidha Rais Samia katika hotuba yake hiyo amesema serikali yake itaboresha sekta mbalimbali ikiwemo kilimo ikiwa kwa kujenga miundo mbinu imara ya kilimo pamoja na kutafuta suala la masoko ili kuwezesha wakulima kufanya kilimo kikubwa na chenye tija bila kusahau sekta ya madini ambayo amesema ataiwekea mkazo mkubwa ikiwemo pia sekta ya viwanda ambayo ni moja ya vitu vilivyopo kwenye ilani ya chama cha mapinduzi, CCM. 

Kadhalika katika hotuba yake Rais Samia amezungumzia suala la Covid-19 huku akisema kuwa Tanzania imejitahidi kupambana janga hilo, na kuwasisitizia wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari za kiafya zinazotolewa na wataalam wa afya. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW