Samia apokea ripoti ya tume ya kuchunguza mzozo, Ngorongoro
13 Machi 2026
Rais Samia Suluhu alipokea ripoti mbili za tume zilizoundwa kuchunguza mgogoro wa hifadhi ya Ngorongoro. Ripoti hizo zimebaini kuwa wananchi hawakushirikishwa vya kutosha, kukosekana kwa sheria na sera zinazoongoza mpango wa kuwahamisha wakazi hao, na mpango wa kuwahamisha ukitumia zaidi ushawishi badala ya utashi.
Hata hivyo Rais akiwa jijini Dodoma, alisema serikali itaendelea na mpango wa kuwahamisha wakazi hao kwa kutumia mfumo unaosisitiza hiari ya wananchi na ushirikishwaji mpana wa jamii.
Mgogoro wa hifadhi ya Ngorongoro ulisikika kwa mara ya kwanza mwaka 2022 baada ya wakazi wanaoishi eneo la hifadhi ya Ngorongoro wengi wao wakiwa ni jamii ya wamaasai, wakilalamika kuondolewa katika eneo ambamo wameishi kwa miaka mingi.
Baada ya baadhi ya wakazi kuhamishwa katika utaratibu uliotajwa kuwa wa hiari, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walihamia Tanga, Msomera lakini kukawepo malalamiko zaidi ya uvunjwaji wa haki za binadamu ikiwamo kuhamishwa kwa nguvu.
Mkazi wa Ngorongoro, Kijiji cha Pololek, Kasale Mwaana, ameiambia DW, ripoti za tume zimepigilia muhuri kondolewa kwa wamasai Ngorongoro.
Desemba 2024, Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume mbili ya Dk Gerald Ndika na ya Jaji Musa Iyombe kuchunguza mgogoro huo uliovutia wanaharakati wa mazingira wa kimataifa na watetezi wa haki za binadamu.
Mkazi mwingine wa Ngorongoro, Nain Tipap, anasema, ripoti hiyo haijagusa maslahi ya wananchi.
Ripoti hizo zimebainisha kuwa mpango wa awali wa kuwahamisha wakazi wa Ngorongoro haukufanikiwa kwani kaya zilizofanikiwa kuhama ni 1678, kati ya kaya 23,000 zinazoishi Ngorongoro huku akibainisha zaidi kuwa kuna nyumba 1559 zilizojengwa Msomera Tanga, ambazo hazijapata wakaazi.